Balozi wa India nchini Tanzania, Debnath Shaw
Wakati Watanzania wakiilalamikia Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma kuwa ni mzigo kwa taifa kwa vile haina meno ya kuwashughulikia wanaokataa kutaja mali, Balozi wa India nchini, Debnath Shaw anasema kwao usipotaja mali unashtakiwa.
“Sielewi vizuri sababu za Tanzania kutowashtaki mahakamani viongozi wanaokataa kutaja mali, labda ndivyo mnavyotaka, lakini nchini kwetu mali za viongozi ziko wazi, tena iko tovuti maalumu ambayo viongozi huandikwa mali zao, sisemi sheria zenu mbaya, bali ni maamuzi yenu Watanzania kuangalia,” alisema Shaw katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari hii jana ofisini kwake.
Hapa nchini iko sheria inayowataka viongozi kutangaza mali zao, hata hivyo, hakuna rekodi yoyoye inayoonyesha kama kuna kiongozi yeyote nchini aliyewahi kufikishwa mahakamani kwa kukataa kwake kutaja mali alizonazo.
Hali kadhalika mali zinazotangazwa haziko wazi kwa wananchi, hata mtu anapokwenda ofisi za tume ya maadili ili kujua kiongozi gani anamiliki nini, hatakiwi kudurufu alichokiona wala kutangaza, hivyo kuondoa maana au umuhimu wa chombo hicho.
India yakataa kuikopesha tena Tanzania
Balozi huyo pia alizungumzia taarifa za India kukataa kuikopesha tena matrekta Tanzania akisema “Hatujakaa kutoa mkopo kwa sababu nyingine zozote, bali mkopo una taratibu zake”.
Hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alilitaka Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT), kulipa deni.Serikali za India na Tanzania ziliingia mkataba wa mkopo wa Sh40 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa matrekta ambayo yalikabidhiwa kwa Suma JKT, hata hivyo kumekuwa na kashfa za baadhi ya vigogo kunufaika isivyo halali na matrekta hayo, tofauti na ilivyolengwa kwamba yangekopeshwa zaidi wananchi wa kawaida wanaojihusisha na kilimo.
Mkopo huo uliosainiwa mwaka 2010 utadumu kwa miaka mitano huku Tanzania kupitia Suma JKT, ikitakiwa kulipa Sh42 bilioni ikiwemo riba.
Hadi sasa Suma JKT imekusanya Sh16 bilioni ambazo ni kiasi kidogo ikilinganishwa na ukubwa wa deni, jambo ambalo Kikwete alikiri lingeweza kuifanya isikidhi vigezo vya kukopeshwa tena.
Hivi karibuni Tanzania iliomba tena mkopo, lakini India ilikataa. Balozi alipoulizwa kama kutolipwa madeni kwa ufasaha ni sababu ya kutokopeshwa tena alijibu kwa kifupi “Nafikiri madeni yanapolipwa, tutapata nguvu za kukopesha zaidi”.
Alipoulizwa kuhusu Serikali kuwa na deni kubwa, hivyo kuwekewa vikwazo vya kupewa mikopo, Waziri wa Fedha, William Mgimwa alisema kuwa jambo hilo analifahamu na kutaka atafutwe leo mchana ili aweze kulitolea ufafanuzi.
Mgimwa ambaye ni mbunge wa Kalenga alisema, “Kwa sasa niko jimboni, ila kuhusu hili suala la Suma JKT naomba unitafute kesho (leo) mchana tutazungumza na kukupa ufafanuzi zaidi.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment