ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 3, 2013

Bodaboda 50 wanaodaiwa kuua waachiwa

Picha hii ni kielelezo cha Bodaboda na watu hawa hawahusiani na mauaji yaliyoelezwa hapa chini

Zaidi ya waendesha bodaboda 50, waliokuwa wakishikiliwa katika kituo cha polisi cha Stakishari wilayani Ilala jijini Dar es Salaam, kwa wiki moja wakikabiliwa na tuhuma za kuua, wameachiwa kwa masharti ya kuripoti kituoni hapo.

Akizungumza na NIPASHE jana, mmoja wa ndugu wa waendesha bodaboda hao ambaye aliomba jina lake lisiandikwe gazetini, alisema baada ya kusota kwa muda mrefu katika kituo hicho hata kususia kula ili waachiwe huru, hatimaye jeshi hilo liliwapa masharti na kuwatoa nje.

“Ndugu zetu hivi sasa wapo nje baada ya kushikiliwa kwa wiki moja, lakini wameambiwa waende kuripoti kituoni hapo hadi ukweli utakapofahamika,” alisema ndugu huyo.Alidai tukio lililowaweka mahabusu waendesha bodaboda hao, linasemekana kutokea Februari 19 mwaka huu, saa 7 usiku wakati gari aina ya Toyota Prado lililokuwa na watu wawili ndani yake, walitaka kukodi bodaboda iwapeleke sehemu, lakini walitiliwa mashaka kutokana na wao kutaka kuliacha gari na kukodi usafiri huo.

“Walishituka kutokana na bodaboda nyingi kuibiwa na watu wanaojifanya abiria na madereva wake kuokotwa wakiwa wameuawa…lakini waligoma baada ya kuamini watu hao si wema kutokana na muda waliofika kituoni tena wakiwa na gari,” alisema.

Hivyo, baada ya bodaboda nyingi kulizunguka gari hilo, dereva wake aliamua kulitoa kwa kasi na kukimbilia maeneo ya Mongo la Ndege ambako huko aliparamia ukuta na kutoweka zake, lakini ikadaiwa mwenzake alikamatwa na kupigwa kisha kupoteza maisha.

“Ilidaiwa baada ya kuuliwa mtu huyo, aliwekwa ndani ya Prado hiyo na kisha kupigwa moto na kuteketeza mwili huo pamoja na gari lote,” alisema ndugu huyo.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Ilala, Marietha Minangi, alikiri kuwepo kwa tukio hilo, ila akasema wahusika wanadaiwa kujihusisha na matukio ya uhalifu.

Aliongeza baada ya dereva wa gari kuingiwa na hofu juu ya kundi la waendesha bodaboda hao, katika jitihada za kujiokoa aligonga ukuta wa jengo la ndege ndipo akatoka na kukimbilia kusipojulikana na kumuacha marehemu ndani ya gari.

“Walichokifanya wale waendesha bodaboda baada ya kumkuta mmoja wao walichukua jukumu la kumuua pale pale na gari yao kuichoma moto” alisema Minangi.  
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: