ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, March 3, 2013

Mgawo wa umeme sasa ni danadana, Pinda aingilie kati

Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika

Tatizo la kukatikati kwa umeme linaloendelea nchini, limeelezwa kusababishwa na mbinu chafu zinazofanywa na kampuni ya ufuaji umeme ya Songas, baada ya Serikali kuikatalia kuongeza ukubwa wa bomba la kusafirisha gesi.

Habari za uhakika kutoka Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco) zimeeleza kuwa, kampuni hiyo ilipoanza kuwekeza nchini, iliombwa kuongeza ukubwa wa bomba hilo kukidhi mahitaji ya umeme, lakini ilikataa.

Wakati hali ikiwa namna hiyo, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, John Mnyika amemtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuingilia kati suala hilo.

Chanzo cha NIPASHE Jumapili kilieleza kuwa, hatua ya Serikali iliishtua kampuni ya Songas iliyoitafsiri kama njia ya kuwakosesha biashara.

“Hapo walianza kufanya ushawishi kwa wabunge na wadau wengine ili yenyewe (Songas) ishiriki kuweka bomba kubwa badala ya Serikali,” kilieleza chanzo hicho.Meneja Uhusiano wa Tanesco, Badra Masoud, alipoulizwa kuhusu shirika hilo kudaiwa na Songas, alithibitisha ingawa hakutaka kuingia kwa undani zaidi.

“Ni kweli wanatudai, lakini kwani hii ni mara ya kwanza kutudai, mbona kuna kampuni nyingi tunazofanya nazo biashara zinatudai, tena fedha nyingi, lakini kutokana na mikataba yetu hakuna sababu ya kulalamika kwenye vyombo vya habari,” alisema.

Aliongeza, “hao Songas mbona wamelipwa juzi mabilioni ya fedha na hawakwenda kwenye vyombo vya habari,” alisema.

Taarifa zaidi zilieleza kuwa kukamilika kwa bomba kubwa la gesi, kutawezesha kupunguza gharama za umeme.

Kwa mujibu wa chanzo hicho, Benki ya Dunia ni miongoni mwa taasisi za kimataifa zilizoonyesha kufurahishwa na mradi huo wa serikali.

Kwa mujibu wa mtoa habari huyo, Songas inafikia kuizimia Tanesco umeme kila mara, ikidai kuna hitilafu kwenye mitambo yake, lakini hawafanyi hivyo kwa wateja wanaowapelekea nishati hiyo moja kwa moja.

Wiki iliyopita, Songas kupitia kwa Fundi Mkuu wake, Dk. Michael Mngodo, ilidai kuwa inashindwa kutekeleza majukumu yake ya kila siku kutokana na kukosa fedha ambazo hazijalipwa na Tanesco.

Mngodo alidai kuwa kwa takribani miezi sita, Tanesco haijawalipa na hivyo kusababisha kushindwa kufanya matengezo katika baadhi ya mitambo yake.

Kwa upande wake, Waziri Kivuli wa Nishati na Madini John Mnyika, amekosoa matamko ya wizara na Tanesco kuhusu mgawo wa dharura wa umeme. Badala yake ametoa wito kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuingilia kati suala hilo ili kupata suluhu iliyo bora.

Alisema wizara ya Nishati na Madini na Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) kwa nyakati tofauti, walitoa majibu yanayokinzana kuhusu mgawo wa dharura wa umeme mwezi huu.

Katibu Mkuu wa Wizara Eliackim Maswi na Afisa Habari wa Tanesco, Badra Masoud wamekaririwa wakisema hakuna mgawo wa umeme, bali matatizo madogo ya mitambo ya gesi.

Mnyika alisema kwa mujibu wa taarifa alizonazo, mgawo wa umeme uliopo unatokana na upungufu zaidi wa kina cha maji katika mabwawa ya kufua umeme.

Pia kuna upungufu wa fedha za kununua mafuta mazito ya kuendesha mitambo ya kufua umeme wa dharura na upungufu wa gesi asili ya kuendeshea mitambo ya kufua umeme.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments: