ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 9, 2013

Denmark kusaidia Monduli milioni 500

Helle Thorning Schmidt 
Waziri Mkuu wa Denmark
Serikali ya Denmark, imeahidi kutoa Sh. milioni 500 kwa ajili ya kujenga bwawa la maji ya kunywa katika kijiji cha Nanja, wilayani Monduli.

Ahadi hiyo imetolewa jana na Waziri Mkuu wa Denmark, Helle Thorning Schmidt, wakati alipotembelea boma la kimasai lililopo kijiji cha Nanja.

Alisema anaamini bwawa hilo litanufaisha vijiji vya kata ya Lepurko yenye vijiji vya Nanja na Mti mmoja.

Helle alisema serikali yake imesikitishwa sana kuona kinamama wa jamii ya wafugaji wanatembea umbali mrefu kusaka maji ambayo si salama.“Kinamama bado wanapata shida wanapokuwa njiani
 kutafuta maji ya kunywa, bado wanakumbana na wanyama wakali kama Simba na wengine kujeruhiwa na baadhi kufariki,” alisema. Alisema anaamini kukamilika kwa bwawa hilo kutawaondolea adha ya maji waliyonayo na kutembea mwendo mrefu kutafuta maji.
Helle alisema serikali yake inajali maendeleo ya wanawake na kutambua mchango mkubwa wa wanawake katika maendeleo.

Alisema hapendezwi kuona akina mama, wakiwa na watoto mgongoni, wanakwenda kutafuta maji kwa mwendo mrefu, hivyo atashughulikia tatizo hilo haraka.

Akiongea kwa niaba ya wenzake, Esuphat Laizer, alisema kuwa kilio cha ukosefu wa maji cha miaka mingi na kutokana na adha hiyo, wamepoteza mwezao mmoja kwa kuliwa na simba kwa sababu ya kutafuta maji na wengine kujeruhiwa.

Alimshukuru waziri huyo na serikali yake kwa msaada huo, ambao walisema utaleta ukombozi mkubwa kwa akina mama kufanya kazi za kujikwamua kiuchumi, badala ya kutumia muda mwingi kutafuta maji.
CHANZO: NIPASHE

No comments: