Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibrod Slaa ameanza kuisakama Idara ya Usalama wa Taifa kuwa wanatumia mbinu mbalimbali kuwahujumu na kwamba mbinu zinazofanywa na idara hiyo ni kueneza propaganda walizodai za uongo dhidi yao.
Akizungumza jana makao makuu cha chama hicho jijini Dar es Salaam, Dk Slaa alisema: “Tumezibaini mbinu zinazofanywa na Usalama wa Taifa kwa kutumiwa na CCM kueneza propaganda za uongo dhidi yao kwa lengo la kukichafua chama, lakini haziwezi kufanikiwa kwani tayari tumegundua mbinu zao.”
“Chadema ni chama makini na hakiwezi kuyumbishwa na mtu yoyote wala idara yoyote inayotumiwa na baadhi ya watu ili kutaka kukizohofisha,” alisema Dk Slaa ambaye mara kwa mara amekuwa akilalamika kuchezewa rafu.
Hata hivyo, viongozi wanaohusika na idara hiyo akiwamo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika walipotafutwa na gazeti hili kwa nyakati tofauti ili kuzungumzia tuhuma hizo za Dk Slaa, hawakuwa tayari kuzizungumzia.
Waziri Mkuchika alisema asingeweza kuzungumzia tuhuma hizi kwa kuwa hakuwa amezisikia wala hafahamu ni ujumbe upi uliomo katika kauli ya Dk Slaa.
“Mimi nimeshinda kwenye Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala tangu asubuhi na sasa ndiyo natoka, kwa hiyo sijasikia hiyo kauli wala huo mkutano wa (Dk Slaa). Kwa hiyo siwezi kujibu chochote kwa sasa,” alisema Mkuchika na kuongeza:
“Nadhani tumeelewana na pengine tusubiri pindi nitakapofahamu ni kipi amekizungumza na nikafanyia uchunguzi tutaona kama kuna cha kujibu basi tutajibu wakati huo, lakini kwa sasa siwezi kusema chochote.”
Mapema gazeti hili lilimtafuta Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Rashid Othman ili kuzungumzia madai hayo ya Chadema lakini mara zote simu yake ilikuwa haipatikani.
Baadaye Mwananchi iliwasiliana na Naibu Mkurugenzi wa Usalama wa Taifa, Jacky Nzoka ambaye alijibu kwa kifupi na kukata simu: “Mimi siyo msemaji tafadhali.”
Hata hivyo, katika tuhuma hizo Dk Slaa alisema mifano hai ipo kwake kwani kila wakati amekuwa akizungukwa na watu wa idara hiyo kwa malengo yao binafsi, lakini malengo yao hayawezi kufanikiwa kwani wao wapo makini katika hilo.
“Mimi kila wakati Usalama wa Taifa wamekuwa wakinizunguka zunguka kwa mambo yao binafsi wanayoyafuatilia kwangu, lakini nataka niwaambie kwamba nimewagundua na mbinu zao haziwezi kufanikiwa ila nawataka wasichoke kunifutalia na waendelee tu,” alisema.
Chadema na Sh400 milioni
Dk Slaa alikiwakilisha Chadema kusaini mkataba wa ushirikiano na Chama cha Konservative cha Denmark ili kuinua uwezo wa vijana na wanawake kisiasa.
Chama hicho kimeahidiwa kupewa Sh400 milioni kwa ajili ya kutoa mafunzo ya kujiimarisha kisiasa kwa Baraza la Vijana la chama hicho (Bavicha) na lile la Wanawake (Bawacha).
“Sisi leo tunasaini mkataba huu, lakini hatuufanyi siri kama vyama vingine vinavyofanya kwani mkataba huu upo wazi na kwamba kila mtu atakayetaka kuona atapewa,” alisema.
Alisema mafunzo hayo yatatolewa kwa watu 900 wa Bavicha na 900 wengine kutoka Bawacha na yanatarajia kuanza siku chache zijazo hadi Desemba mwaka huu yakiwa na lengo la kuwajengea uwezo wa kisiasa vijana wa Chadema na wanawake ili kuhakikisha wanaimarika kisiasa Tanzania,” alisema Dk Slaa.
Akizunguza wakati wa kusaini mkataba huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kimataifa ya Chama cha Conservative, Rolf Aagaard-Svendsen alisema lengo la ushirikino wao ni kuwajengea uwezo wa kisiasa vijana ili washiriki vizuri katika medani za kisiasa.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment