ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, March 5, 2013

Hakimu: Ponda ana kesi ya kujibu



  Wenzake nao wana kesi
  Kuanza kujitetea kesho
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Jijini Dar es Salaam imesema washtakiwa wote 50 akiwamo Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Sheikh Ponda Issa Ponda (54) wana kesi ya kujibu katika kesi ya kula njama, kuingia, kujimilikisha ardhi kwa jinai na wizi wa mali ya Sh. milioni 59.6.
 
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi, Victoria Nongwa, baada ya kupitia ushahidi uliotolewa na mashahidi 17 wa upande wa mashtaka na mahakama imewaona washitakiwa wanastahili kusimama kizimbani na kuieleza kuhusiana na mambo kadhaa yaliyojitokeza.
 
Alisema washtakiwa wanatakiwa kujitetea kwanini walikutwa katika eneo la Chang’ombe Marcas, jijini Dar es Salaam na ni jukumu lao kuieleza mahakama kuhusu maswali hayo.
 
“Washtakiwa mnatakiwa kujitetea na kuieleza mahakama kwa nini mlikamatwa katika eneo la Chang’ombe Marcas ili kuiondolea maswali yaliyopo kutokana na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri dhidi yenu,” alisema Hakimu Nongwa na kuongeza:
 
“Inaonekana kuwa baadhi ya Waislamu hawakuridhika na kubadilishana ardhi kati ya Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) na Kampuni ya Agritanzan Ltd. Kutokana na hilo, mahakama haimzuii mtu yoyote kwenda kwenye chombo husika kinachoshughulikia masuala ya ardhi ikiwamo Mahakama ya Ardhi,” alisema Hakimu Nongwa.
 
Akifafanua zaidi, hakimu huyo alisema kuwa baada ya uamuzi huo, washtakiwa wataanza kupanda kizimbani kujitetea kuanzia kesho.
 
Mbali na Ponda, washtakiwa wengine ni Sheikh Mukadam Saleh, Kuluthumu Mohamed, Zaldah Yusuph, Juma Mpanga, Farida Lukoko, Adamu Makilika, Athum Salim, Seleman Wajumbe, Salum Juma, Salum Mkwasu na Ramha Hamza.
 
Wengine ni Halima Abas, Maua Mdumila, Fatihiya Habibu, Hussein Ally, Shaban Ramadhani, Hamis Mohamed, Rashid Ramadhani, Yusuph Penza, Alawi Alawi, Ramadhani Mlali, Omary Ismaili, Salma Abduratifu, Khalidi Abdallah, Said Rashid, Feswali Bakari, Issa Wahabu, Ally Mohamed, Mohamed Ramadhani, Abdallah Senza, Juma Hassani na Mwanaomary Makuka.
 
Wengine ni Omary Bakari, Hamza Ramadhani, Ayubu Juma, Maulid Namdeka, Farahan Jamal, Smalehes Mdulidi, Jumanne Mussa, Salum Mohamed, Hamis Halidi, Dite Bilali, Amiri Said, Juma Yassin, Athuman Rashid, Rukia Yusuph, Abubakari Juma na Ally Salehe.
 
Upande wa wa mashtaka ulidai kuwa, katika shtaka la kwanza Oktoba 12, mwaka huu huko Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote 50 walikula njama za kutenda makosa.
 
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa siku ya tukio la kwanza katika eneo la Chang’ombe Markas, Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam, washtakiwa wote 50 kwa jinai walivamia kwa nia ya kutaka kujimilikisha kiwanja ambacho ni mali ya Agritanza Ltd.
 
Ilidaiwa kuwa katika shtaka la tatu, kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu huko Chang’ombe Markas pasipo uhalali na hali ya uvunjifu wa amani, washtakiwa wote walijimilikisha ardhi ambayo ni mali ya Agritanza Ltd.
 
Katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu eneo la Chang’ombe Markas, washtakiwa wote waliiba vifaa mbalimbali vya ujenzi ikiwamo matofali 1,500, tani 36 za kokoto na nondo vyote vikiwa na thamani ya Sh. 59,650,000 mali ya Agritanza Ltd.
 
Upande wa Jamhuri ulidai kuwa shtaka la tano linamkabili Sheikh Ponda na Mkadam, kati ya Oktoba 12 na 16, mwaka huu katika eneo la Chang’ombe Markas, Sheikh Ponda aliwashawishi wafuasi wake kutenda makosa ya jinai.
 
Washtakiwa wote walikana mashtaka dhidi yao kwa nyakati tofauti.
Oktoba 18, mwaka huu, washtakiwa hao walifikishwa katika mahakama hiyo kwa mara ya kwanza na kusomewa mashtaka, lakini Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), aliwasilisha hati ya kiapo cha kupinga dhamana ya Sheikh Ponda na Mukadam kwa usalama wao na maslahi ya taifa.
 
KESI YA WAANDAMANAJI YAKWAMA
 
Wakati huo huo, mahakama hiyo imepiga kalenda kusikiliza ushahidi wa washtakiwa 54 wanaokabiliwa na mashtaka ya kula njama na kufanya maandamano isivyo halali hadi leo.
 
Kesi hiyo ilishindwa kusikilizwa jana kutokana na wakili wa upande wa Jamhuri kushindwa kufika mahakamani kwa kuwa alikuwa anaumwa.
 
Hakimu Sundi Fimbo aliahirisha kesi hiyo hadi leo na washtakiwa wataendelea kujitetea.
 
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Salum Makame, Said Idd na Ally Nandumbi, Makame, Idd na Nandumbi, Hussein Athuman, Seif Rwambo, Abdull Ally, Waziri Swed, Naziru Waziri, Ahmad Rashid, Jumanne Kayogola, Hamis Tita, Amri Diyaga, Salum Said, Rajabu Mpita na Haji Sheluhenda.
 
Wengine ni Abdul Ahmed, Bakari Mwambele, Ramadhani Fadhili, Awadhi Juma, Omari Mkwau, Kassim Chobo, Abubakari Bakari, Ramadhani Milambo, Hamis Ndeka, Athuman Juma, Abdallah Salum, Juma Makoti, Bashir Kakatu, Imam Omari, Rashid Lukuta na Bakari Athuman.
 
Wamo pia Mbwana Kassim, Nurdin Ahmed, Mustapha Mide, Rajabu Kifumbo, Zuberi Juma, Omari Mkandi, Idrisa Katulimo, Sawali Mola, Said Dudu, Ramadhani Juma, Musa Sinde, Issa Sobo, Yahaya Salum, Jabil Twahil, Shomari Tarimo, Hashim Bendera, Waziri Toy, Athuman Yahaya, Yasin Seleman, Shaban Malenda, Yasin Mohamed, Khatib Abdallah na Rajabu Rashid, wote wakazi wa jijini Dar es Salaam.
 
Ilidaiwa kuwa, Februari 15, mwaka huu katika wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam, washtakiwa walikula njama ya kufanya maandamano isivyo halali.
 
Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa siku na eneo la tukio la kwanza washtakiwa walifanya mkusanyiko usio halali kwa lengo la kusababisha uvunjifu wa amani.
 
Wakili huyo wa Jamhuri, Nassoro Katuga, alidai kuwa katika shtaka la tatu  siku na eneo la tukio la kwanza na la pili, washtakiwa wote baada ya Jeshi la Polisi kutoa zuio la kufanya maandamano, walikiuka amri hiyo na kufanya mkusanyiko ulisababisha vurugu na uvunjifu wa amani.
 
Katika shtaka la nne, ilidaiwa kuwa washtakiwa Makame, Idd na Nandumbi waliwashawishi wananchi kwa kuwasambazia vipeperushi vya kuhamasisha kufanya maandamano yasiyo halali.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: