ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 7, 2013

Hugo Chaves: 'Nyerere' wa Venezuela aliyetabiriwa kifo na daktari wake.

Rais wa Venezuela, Kamanda Hugo Chavez kama ambavyo wenyewe hupenda kumuita, hatunaye tena duniani, wananchi wa taifa hilo la Amerika ya Kusini bado wanajiuliza kuhusu mustakabali wao.

Hakuna ubishi kwamba Kamanda Chaves alikuwa mioyoni mwa wananchi wengi wa taifa hilo tajiri kwa mafuta, ingawa hakukukosekana watu wanaompinga.

Siasa zake za ujamaa ndizo zilimpa umaarufu zaidi nchini mwake na namna alivyokuwa mkosoaji mkubwa wa siasa za kibepari hasa akiwa mpinzani mkubwa wa Marekani. Kamanda Chaves aliyetawala taifa hilo kwa miaka 14 mfululizo, alipendwa na wananchi wake kwa namna alivyokuwa akihakikisha rasilimali za taifa hilo zinatumika kwa maslahi ya wananchi wote.
Alitumia fedha zinazotokana na mafuta kusamabaza huduma za jamii katika maeneo mengi ya nchini mwake na hakuwa na tamaa ya kujilimbikizia mali kama tunavyoshuhudia viongozi wengi wa Afrika.

Wachambuzi wa mambo wanasema ingawa alikuwa hasimu wa Marekani, lakini nchi hiyo ilikuwa mnunuzi mkubwa wa petroli ya Venezuela.

Tangu achaguliwe kuongoza muhula wa tatu mwishoni mwa mwaka jana, Rais wa Hugo Chavez hakuwahi kuonekana hadharani kutokana na maradhi ya saratani yaliyomsumbua kwa muda mrefu.

Alirejea mjini Caracas Februari 18 kwa mara ya kwanza na alipelekwa hospitali ya kijeshi kuendelea kupata matibau lakini alifariki dunia Machi 5, akiwa hospitalini hapo.

Wasifu wa Chavez
Hugo Chavez alijitosa katika siasa za Venezuela mnamo Februari 1992 akiwa Luteni katika Jeshi. Aliongoza mapinduzi dhidi ya rais wa wakati huo Carlos Andres Perez.
Lakini kutokana na kukosa usaidizi wa kutosha wa kijeshi, Chavez na wanamgambo wenzake walishindwa kunyakua madaraka hayo na aliwekwa korokoroni.

Aliingia madarakani baada ya ushindi mkubwa ulioviondosha vyama vya kisiasa wakati huo na wakati wa kuapishwa kwake Februari, 1999, Chavez alitangaza wazi kwamba mipango yake ya mabadiliko ya kisiasa na kiuchumi sio kampeni tu.

Alitimiza ahadi yake na kuiongoza nchi hiyo katika mabadiliko ambayo hayakuwahi kushuhudiwa katika muda wa miongo kadhaa ambapo alibadili muundo wa Bunge na kulifanya kuwa la kikatiba, ambalo liliiunda Katiba mpya baada ya kura ya maoni iliyoidhinishwa na 88% ya wapiga kura.

Rais Chavez alitaifisha rasilmali ukiwemo utajiri wake mkubwa wa mafuta. Sera kama hizo zilimfanya azozane na kampuni za kimataifa za mafuta, lakini alipata uungwaji mkono mkubwa wa watu maskini.

Chavez na jamii ya kimataifa
Kutokana na urafiki wake na viongozi wa mrengo wa kushoto kama vile rais wa Cuba, Fidel Castro, ambaye walikuwa na uhusiano wa karibu aligongana kidiplomasia na Marekani, ambayo ni mshirika wake mkuu wa kibiashara.

Chavez alipendwa nyumbani na wafuasi wake lakini alipingwa na baadhi ya watu nchini humo na katika nchi za nje. Alionekana sio tu kama bingwa wa jamii maskini lakini pia kama muingiliaji wa siasa za nchi jirani na katika miaka ya hivi karibuni alilenga kukabiliana na masuala ya ndani ya Venezuela, kama uhalifu, kuinua uchumi wa nchi na kukabiliana na rushwa.

Kuugua kwake kulileta utata wa kikatiba ambayo ilitaka awe ameapishwa Januari 10, lakini wakati huo alikuwa kwenye matibabu nchini Cuba ambako alikaa tangu Desemba 11 mwaka jana.

Chavez hakuwahi kuonekana hadharani na tangu alipofanyiwa upasuaji wa nne uliotokana na ugonjwa wa saratani Desemba 11, mwaka jana.

Serikali ya Venezuela ambayo kwa muda mrefu ilishindwa kuzungumzia afyaya kiongozi huyo, hatimaye baada ya afya ya kongozi huyo kuwa mbaya ilivunja ukimya na kutangaza kuwa tatizo la kushindwa kupumua la rais Hugo Chavez limekuwa baya zaidi na anaumwa maambukizi makali ya pumu.

Katika taarifa iliyotolewa kwenye Televisheni ya taifa na Waziri wa Habari , Ernesto Villegas, alisema Kamanda Chavez yuko mahututi.

Rais huyo wa Venezuela ambaye wakati mmmoja alikuwa ndiye nguzo kuu ya Amerika kusini saa za mwisho za uhai wake alikuwa anatumia mirija ili kumsaidia kupumua.

Wapinzani wake walikuwa wakiuchukua ugonjwa wake kama karata yao kisiasa kwa kumzushia kifo na kutaka uchaguzi huru, hali ambayo inapingwa vikali na washirika wa Chavez.

Wasaidizi wake wa karibu pamoja na ndugu wa Chavez walikuwa wakikanusha habari kuwa rais huyo anaweza kuwa amefariki au anakaribia kufa kutokana na ugonjwa wa saratani na kusema kuwa bado anapigana kuokoa maisha yake.

Makamu wake, Nicolas Maduro alisema wiki iliyopita kuwa Chavez yuko katika hali nzuri, lakini akipigania maisha yake wakati akifanyiwa tiba ya kutumia kemikali katika hospitali ya kijeshi mjini Caracas.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Maduro kutangaza kuwa rais huyo ameanza kutumia tiba hiyo ya kemikali kufuatia upasuaji wa nne wa saratani nchini Cuba mwezi Desemba mwaka jana, na kuamua kuendelea na matibabu nchini kwake.

Alisema Chavez na madakatari wake waliamua kuanza tiba ya kemikali na mionzi, baada ya hali yake kuboreka mwezi Januari mwaka huu.

Habari za kifo cha Chavez
Minong'ono kuhusu afya ya rais Chavez ilifikia kiwango cha juu wiki iliyopita, kufuatia madai ya balozi wa zamani wa Panama katika Umoja wa Mataifa ya Amerika OAS, Guillermo Cochez, kuwa kiongozi huyo wa Venezuela alikuwa amefariki.

Mkwe wa Chavez Jorge Arreaza alikosoa matamshi hayo ya Cochez na kusema ni habari za uongo zinazosambazwa na wafuasi wa mrengo wa kulia na kwamba kama hawajui hilo linawaharibia wao wenyewe kwa kuzidi kuwatenga na watu, na kuongeza kuwa rais Chavez alikuwa ametulia hospitalini.

Picha za hivi karibuni zilimuonyesha Chavez akiwa hospitalini akiwa amezungukwa na mabinti zake.

Wiki iliyopita Chavezi alifanya uamuzi wa kushtukiza na kurudi Venezuela, lakini bila mbwembwe kama zilizokuwepo wakati akirejea nyumbani baada ya matibabu katika nyakati zilizopita akitokea huko huko Cuba.

Makamu wake, Maduro, kiongozi asiye rasmi wa taifa hilo mwanachama wa Jumuiya ya Mataifa yanayozalisha mafuta kwa wingi OPEC na aliyependekezwa na Chavez kuwa mrithi wake, aliwataka wavenezuela kuwa watulivu, wavumilivu na waheshimu hali aliyo nayo rais wao.
"Tiba anayopokea kamanda Chavez ni kali, lakini ana nguvu kuishinda," Maduro alisema baada ya misa ya Katoliki aliyofanyiwa Chavez katika kanisa lililoko hospitalini, kabla ya Chavez hajafariki.

Upinzani wailaumu serikali
Wanasiasa wa upinzani walikuwa mara kadhaa wakiishtumu serikali kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu hali ya Chavez na walilinganisha usiri wa taarifa za afya ya Chavez na uwazi ulioonyeshwa na viongozi wengine wa Amerika Kusini walioumwa ugonjwa wa saratani.

"Maduro ameendela kuwadanganya wafuasi wa rais na wavenezuela wote kuhusu hali yake halisi lakini ngoja tuone atakavyolielezea taifa katika siku zijazo uongo wote alioutoa,"alisema

Mwandiplomasia wa Panama Cochez alisema ndugu zake Chavez walimuondolea mashine za kupumua siku nyingi zilizopita, baada ya kuwa katika hali ya kutojitambua tangu mwishoni mwa mwezi Desemba. Alisema kama maofisa wa serikali wanasema anayozungumza ni uongo basi wamwonyesha uongo wake kwa kumuonyesha rais Chaves hadharani.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

10,000 kwa siku hii ni Tanzania au?