ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 9, 2013

Jopo la madaktari wanne wamtibu Kibanda

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda anatibiwa na jopo la madaktari wanne katika Hosipitali ya Millpark nchini Afrika Kusini.
Juzi madaktari hao walibaini madhara zaidi aliyoyapata mwenyekiti huyo kutokana na unyama aliofanyiwa na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia jumatano wiki hii.
Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa magazeti yaliyopo chini ya Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, alitekwa, kupigwa na kujeruhiwa vibaya na  alisafirishwa kwenda Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.
Habari ambazo gazeti hili lilizipata kutoka Afrika Kusini, New Habari na  kuthibitishwa na TEF, zilisema madaktari wameanza kutibu majeraha na athari zilizotokana na majeraha, kushughulikia uvimbe katika sehemu mbalimbali za kichwa chake na kuondoa damu iliyovilia.
Taarifa ya TEF iliyotolewa na Katibu Mkuu wake, Neville Meena ilisema lengo la matibabu hayo ni kuwezesha mzunguko wa damu kurudi katika hali yake ya kawaida na kuzuia sehemu nyingine zenye majeraha zisishambuliwe na vijidudu vinavyoweza kusababisha magonjwa mapya.
“Baada ya kutibu majereha na kuondoa uvimbe, madaktari wataeleza hatua za kuchukua kwa maana ya tiba ya ziada iwe ni upasuaji au vinginevyo,” alisema.
Kuhusu tiba ya macho, Meena alisema taarifa zilisema kuwa nalo linasubiri kupungua uvimbe na ushauri wa daktari bingwa wa macho.
“Pia mifupa midogo inayozunguka eneo la jicho nayo imebainika kuwa imeathirika kiasi, kwa jumla hali ya Kibanda inaendelea kuimarika na jopo la madaktari wanne wanaomtibu limesema hakuna shaka kwamba matatizo yake yatapata tiba inayostahili,” alisema.
Kutokana na tukio lililomkuta Kibanda, Jukwaa la Wahariri katika kikao chake cha dharura jana kilichowashirikisha wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari, limeunda tume ya watu watano kufanya utafiti wa kihabari wa tukio hilo.
Timu hiyo itaundwa na wajumbe watatu kutoka TEF na mjumbe mmojammoja kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika, tawi la Tanzania (Misa-Tan).
Timu hiyo itaanza kazi katika muda wa wiki moja kuanzia sasa na itafanya kazi hiyo kwa wiki mbili, taarifa ya utafiti huo ndiyo itakuwa mwongozo wa  hatua za kuchukua kutokana na tukio hilo.
Kibanda alitekwa  na watu wasiofahamika na kisha kumjeruhi vibaya kwa nondo, mapanga na kisha kumng’oa meno mawili, kucha na kumharibu jicho la kushoto

Mwananchi

1 comment:

Anonymous said...

Kwani angebaki muhimbilimbili angetibiwa na daktari mmoja? Wengi tunaelewa kuwa madaktari wame-specialize katika magonjwa wanayotibu. kwanini jopo la maktari inakuwa ni "news"