ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 29, 2013

KAMA UMESALITIWA, FANYA HAYA KABLA YA KUMUACHA!

Suala la wapenzi au wanandoa kusalitiana limekuwa likiwaumiza walio wengi na baadhi wanaposalitiwa hujikuta wakichanganyikiwa na wengine kuchukua maamuzi ya kukatisha maisha yao.

Hakuna anayeweza kusema kuwa, haumii anaposalitiwa na kama yupo basi huyo aliyenaye hampendi kwa dhati.

Kama unampenda, akikusaliti lazima utaumia lakini cha kujiuliza ni kwamba, tukishasalitiwa ndiyo mwisho wa maisha yetu? Tukisalitiwa na wapenzi wetu suluhisho ni kunywa sumu?

Sidhani kama hayo ni maamuzi ya busara. Yapo ya kufanya unapokumbwa na balaa hili la kusalitiwa na leo nimeona nikupe dondoo chache zinazoweza kukusaidia.
Kwanza, kubaliana na kilichotokea. Kama ameshakusaliti ni tukio ambalo limeshatendeka na huwezi kufanya chochote kulifuta. Kwa maana hiyo kubali kuwa umetendwa na kwa kuwa una moyo wa kibinadamu, huzunika mwisho liache lipite ili uweze kujipanga upya.
Pili, usijalaumu. Kuna ambao wakishasalitiwa huanza kujilaumu ni kwa nini waliingia kwenye uhusiano na watu waliowatenda. Utamsikia mtu akisema; ‘Najuta kumpenda fulani’. Kujilaumu kwa namna hiyo hakutakiwi kwani kutakufanya uzidi kupata maumivu moyoni mwako na kunyong’onyea.
Tatu, jifanye kama vile aliyesalitiwa siyo wewe bali ni rafiki yako kisha jiulize ungemshaurije? Ushauri ambao ungempatia basi uchukue kisha ufanyie kazi.
Kujitoa kwako kwenye tatizo kunaweza kukupunguzia machungu kwa kiasi fulani licha ya kwamba si kazi rahisi.
Nne, je, kitendo cha mpenzi wako kukusaliti kimekukosesha imani juu yake? Kama ni hivyo, unadhani una sababu ya kuendelea kuwa naye au unahisi madhara aliyokupatia huwezi kumvumilia?
Kama utapata jibu ni vyema ukachukua uamuzi ambao nafsi yako itaona ni sahihi.
Tano,usione hatari kumpasha ukweli. Kwa vyovyote utakavyoamua ni lazima umweleze namna alivyokuumiza kwa usaliti wake. Hata kama utampa nafasi nyingine lazima ajue jinsi alivyokuumiza ili iwe changamoto kwake.
Sita, jaribu kuchunguza ili kujua kwa nini amefikia hatua ya kukusaliti. Usiliache likapita hivihivi, unatakiwa kujua sababu ya yeye kukusaliti. Je, kuna ambacho anakikosa kwako au ni tamaa zake tu? Jibu utakalolipata litakusaidia katika maisha yako ya kimapenzi.
Saba, usikubali akuletee usanii katika hilo. Nasema hivi kwa kuwa, huenda huyo mpenzi wako ni ‘mjanjamjanja’ na anaweza kukulainisha kwa maneno ambayo yanaweza kukufanya ukalichukulia poa tukio hilo. Kuwa na msimamo na eleza hisia zako kwa uwazi.
Nane, ni vyema ukachukua uamuzi sahihi. Kama amekusaliti, uamuzi wa kuendelea kuwa naye au kumuacha uuchukue bila shinikizo. Hata kama kakuumiza, kama unadhani unaweza kumpa nafasi nyingine mpe ili usije ukajuta baadaye kwa kumkosa lakini kama unaona moyo wako unasita, muache.
Tisa, unayo nafasi ya kumsamehe licha ya kwamba utakuwa umeachana naye. Hii itakusaidia kuliondoa dukuduku lako moyoni na kujiepusha na kukosa amani.
Kumi, chukulia tukio hilo kama fundisho kwako. Huenda wewe ndiye uliyechangia kusalitiwa, kama ni hivyo badilika ili yasije yakakukuta kama hayo utakapokuwa na mwingine. Pia kama kusalitiwa kumetokana na kutoridhika kwa mpenzi wako, kuwa makini wakati wa kuchagua mwingine wa kuwa naye.
Global Pulishers

No comments: