ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 18, 2013

Kocha: Tatu bora ngumu kwetu

Dar es Salaam. Kocha wa timu ya Tanzania kwenye michuano ya dunia ya mbio za nyika, John Bayo amesema ni vigumu kwa wachezaji wake kuingia hatua ya tatu bora ya michuano hiyo itakayofanyika Jumamosi hii mjini Bydgoszcz, Poland.
Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu kutoka Kenya alipokuwa akishughulikia visa za msafara huo wa Tanzania, Bayo alisema timu yake ina wachezaji wazuri ambao wana uwezo wa kushinda kwenye mbio za mchezaji mmojammoja.
“Kwenye mbio za makundi bado tuna wakati mgumu na ndizo zitakazotukwamisha kuingia hatua ya tatu bora kwani katika timu za Afrika Mashariki tukubali tukatae, Kenya na Uganda hivi sasa wako vizuri kwenye riadha kulinganisha na sisi,” alibainisha kocha Bayo.
“Kwenye kumi bora hakuna shaka tutakuwemo, lakini kuingia tatu bora ni vigumu,” alibainisha kocha huyo na kuongeza kuwa wasiwasi wake mwingine ni hali ya hewa ya nchi hiyo ambayo wiki iliyopita imekuwa na baridi kali.
“Wasiwasi na hali ya hewa ya huko tumesikia barafu ikidondoka ingawa sina shaka na wachezaji kama Dickson Marwa na Damian Chopa, wana uwezo mkubwa na naamini watawaongoza wenzao kwenye mapambano.”

No comments: