ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 21, 2013

Nyerere, Karume watajwa kesi ya wafuasi wa Ponda

Shahidi wa utetezi  na Mwanzilishi wa Baraza la Misikiti Tanganyika, Bilali Waikela (87), amedai mahakamani katika kesi inayomkabili Sheikh Issa Ponda na wenzake 49, kwamba  Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Shekhe Abeid Karume, walivunja Umoja wa Waislamu wa Afrika Mashiriki.

 
Waikela alidai kuwa umoja huo ulianzishwa kwa lengo la kuwatetea na kuwasaidia Waislamu na kwamba Tanzania ilipata kiwanja cha Chang’ombe Marcas kutoka kwa aliyekuwa Rais wa Misri.
 
Waikela ambaye ni shahidi wa 48 wa upande wa utetezi katika kesi hiyo alidai kuwa, umoja huo ulifutwa baada ya Karume kudanganywa kuwa wana mpango wa kufanya mapinduzi na kuwarudisha Waarabu Zanzibar.
 
“Mwalimu Nyerere ndiye aliyemtuma Karume afanye hivyo na mwaka 1964 nilifungwa baada ya kukataa kupokea Shilingi 40,000 ili nikubali kuvunja umoja huo, na  Kassim bin Juma, Adam Simba na Salehe Masasi waliotumiwa kuhamasisha watu kuvunja umoja huo,” alidai.
 
Alidai kuwa ofisi za umoja huo zilifungwa hadi mwaka 1968 lilipoundwa Baraza la Waislamu Tanzania (Bakwata) na kukabidhiwa ofisi pamoja na mali zote kikiwamo kiwanja cha Chang’ombe markazi kilichokuwa kimejengwa shule ya Waislamu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: