ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 21, 2013

Lissu, Mnyika, Nassari wasakwa

Lissu                                  Mnyika                             Nassari
Bunge limesema uamuzi wa kuwahoji wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wanaotuhumiwa kuwa ni vinara wa vurugu bungeni, bado uko palepale.

Vurugu hizo zilitokea bungeni, Februari 4, mwaka huu, wakati Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, alipowasilisha hoja binafsi iliyoitaka serikali kuchukua hatua za kuboresha upatikanaji wa maji safi na ushughulikiaji wa maji taka katika Jiji la Dar es Salaam.


Wabunge waliotuhumiwa kuhusika na vurugu hizo, ni Joshua Nassari (Arumeru Mashariki), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Mnyika na Pauline Gekul (Viti Maalum), ambao wote wanatarajiwa kuhojiwa na Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, inayoongozwa na Mbunge wa Mlalo (CCM), Hassan Ngwilizi. 

Kaimu Mkurugenzi wa Kamati za Bunge, Theonist Luhirabake, alisema jana kuwa iwapo wabunge hao watakataa wito wa kwenda kuhojiwa na kamati hiyo, hatua nyingine zitachukuliwa dhidi yao.

Wiki iliyopita, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, aliliambia NIPASHE kuwa kwa mujibu wa kanuni za Bunge, mbunge anayekaidi wito wa kwenda kuhojiwa, anaweza kukamatwa na kupelekwa kwenye kamati kujibu.

Luhirabake alisema wabunge wote wa Chadema wanaotuhumiwa kuhusika na vurugu hizo, waliitwa hivi karibuni na kamati hiyo na kila mmoja alikabidhiwa hati ya wito wa kwenda kuhojiwa.

“Wote walifika mbele ya kamati, wakakabidhiwa summons (hati ya wito wa kwenda kuhojiwa). Na wote watahojiwa,” alisema Luhirabake.

Alisema wabunge hao walitarajia kuitwa tena ili kuhojiwa na kamati hiyo juzi, lakini imeshindikana kutokana na ratiba ya shughuli za kamati za Bunge zilizoanza rasmi Jumatatu wiki hii kubana.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa lazima wabunge hao watahojiwa na kusema iwapo watakataa kwenda kuhojiwa Bunge litachukua hatua nyingine.

Msimamo huo wa Bunge umetolewa siku chache baada ya Lissu kusema hawatakwenda kuhojiwa na kamati hiyo, akitaja sababu kadhaa, mojawapo ikiwa ni kutotambua uhalali wa kamati hiyo kwa madai kwamba, wakati huo haikuwako kisheria.

Lissu, ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alitangaza msimamo huo saa chache baada ya kukutana na kamati hiyo na kugoma kuhojiwa nayo.

Alisema aligoma kuhojiwa kutokana na kamati hiyo kumpa tuhuma siku hiyo ikiwa ni siku rasmi ya mahojiano, kinyume cha kanuni za Bunge, ambazo alidai zinataka mbunge anapotuhumiwa apewe siku tatu za kujiandaa kabla ya kwenda kuhojiwa.

Alisema alikutana na kamati hiyo kwa dakika 15 na kwamba, aliondoka baada ya kuitolea hoja kadhaa kuhusu utaratibu huo.

Lissu alisema sababu nyingine kuwa ni kwa vile kamati hiyo ilikaa Februari 5 kujadili jambo hilo na Februari 8, mwaka huu, ikatoa hukumu yake mbele ya Bunge kwamba, katika uchunguzi wao wabunge wanne au watano walisababisha vurugu bungeni. Hivyo, alisema kamati hiyo, ambayo kwa sasa inafanya shughuli zake kimahakama, haiwezi kukaa tena kwa jambo hilo.

Alisema hoja hiyo inatiwa nguvu na kifungu cha 280 cha Sheria ya Mwenendo wa Jinai alichosema kinamlinda kwa kuwa tayari alishaachiwa huru na ‘mahakama’, hivyo hawezi kushitakiwa tena kwa kosa hilo hilo moja.

Msimamo huo wa wabunge wa Chadema uliungwa mkono pia na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, na Katibu Mkuu wake, Dk. Willibrod Slaa, ambaye alimuagiza Lissu kumuandikia Spika wa Bunge, Anne Makinda, barua kumhoji amepata wapi mamlaka ya kuita wabunge kuhojiwa na kamati, ambayo imemaliza muda wake.

Hata hivyo, siku moja baadaye, Dk. Kashililah alipingana na madai hayo ya Lissu na kusema kamati hiyo bado iko hai kwa kuwa haikuvunjwa na Spika.

Dk. Kashililah alisema mbunge yeyote atakayekaidi kuitikia wito wa kamati hiyo wa kwenda kuhojiwa anaweza kukamatwa.

Alisema Februari 9, mwaka huu, wakati Bunge linaahirishwa, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alitamka ndani ya Bunge kwamba, amezivunja kamati zote za kudumu za Bunge, isipokuwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge na ile ya Kanuni za Bunge.
Alisema kwa mujibu wa kanuni za Bunge, mwenye mamlaka ya kutafsiri kanuni za Bunge na kuunda na kuvunja kamati za Bunge ni Spika.

Kutokana na hilo, alisema kama kuna mbunge hakuridhika na maamuzi ya Spika ya kutozivunja kamati hizo mbili, alipaswa kufuata utaratibu wa kibunge wa kuandika malalamiko kukata rufaa, badala ya kukimbilia kwenye magazeti.

Akifafanua kuhusu hatua anazochukuliwa mbunge kwa kukaidi kuhojiwa, Dk. Kashililah, alisema kuna utaratibu umewekwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, ambayo alisema itaamua nini cha kufanya.

Alisema utaratibu uliopo ni kwamba, mbunge anaweza kuitwa kwa hati maalum ya wito (summons) au kwa ujumbe wa polisi (police massage).

Akijibu madai kwamba, wabunge hao wanaitwa wakati wameshahukumiwa kwa kuitwa vinara wa vurugu, Dk. Kashililah alisema madai hayo hayana ukweli.

Alisema kama wabunge hao wangekuwa wamehukumiwa kama inavyodaiwa, basi kisheria wangekuwa wamepewa adhabu na kwamba maamuzi dhidi ya tuhuma zinazowakabili wabunge hao bado hayajatolewa.

Dk. Kashililah alisema siku hiyo kamati hiyo ilisema kwa kuwa wabunge hao haikuwaita, basi ili kuwatendea haki na kutoa hukumu ya haki juu yao itawaita na kuwahoji.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments: