Rais wa shirikisho la Soka nchini TFF,Leodgar Tenga (katikati) akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam jana
Hatimaye mgogoro baina ya serikali na TFF umemalizika baada ya serikali kukubali mchakato wa uchaguzi wa shirikisho hilo la soka uendelee pale ulipoishia; jambo linalomaanisha kuwa hoja zote zilizoibuliwa na serikali zikiashiria kuingilia masuala ya soka zimetupwa.
Hakuna agizo hata moja miongoni mwa yaliyotolewa awali na serikali kuhusiana na mgogoro huo ambalo liliridhiwa katika kikao kilichofanyika juzi baina ya pande hizo mbili.
Awali, serikali iliifuta katiba mpya ya TFF ya Desemba 15, 2012 na kuagiza itumike ya mwaka 2006 na iitishe mkutano mkuu wa marekebisho ya katiba ndani ya siku 40 na pia iwe imefanya mkutano mkuu wa uchaguzi kabla ya Mei 25, 2013.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za shirikisho hilo jijini Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga alisema serikali imekubali kuwa mchakato wa uchaguzi wa shirikisho hilo uendelee.
Alisema uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao kati ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo chini ya waziri, Dk. Fenella Mukangara, TFF na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kilichofanyika jijini Dar es Salaam juzi.
Tenga ambaye jana alikuwa amefuatana na Mwenyekiti wa BMT, Dioniz Malinzi na watendaji wengine wa baraza hilo na TFF, alisema kuwa baada ya maafikiano hayo, TFF italiandikia barua Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) ambalo ndilo lililosimamisha mkutano mkuu wa uchaguzi huo baada ya kuombwa na baadhi ya wagombea walioenguliwa, ili litume ujumbe wake kuja kusikiliza malalamiko ya wagombea hao. Awali, uchaguzi huo ulipangwa kufanyika Februari 24.
Tenga pia aliishukuru serikali kwa kuruhusu mchakato huo uendelee na kwamba TFF itahakikisha uchaguzi unafanyika kabla ya Mei 25 mwaka huu kama walivyokubaliana kuwa haki si tu inatendeka bali ionekane imetendeka.
“Serikali imetuelekeza kuwa uchaguzi ufanyike kabla ya Mei 25. Tumewaambia kwetu huko ni mbali. FIFA wakija hata kesho na kutuambia endeleeni, sisi tuko tayari. Hesabu zetu ziko tayari, makabrasha yote yako tayari, yanasubiri mkutano tu... labda itakuwa kutoa muda tu kwa wajumbe walioko mbali waweze kujiandaa, maana wajumbe huwezi kuwaita ghafla,” alisema Tenga.
“Sisi (TFF) tulipanga tarehe ya uchaguzi kuwa Februari 24, lakini ukasimamishwa na FIFA baada ya baadhi ya walioenguliwa kulalamika huko. Hivyo maneno kuwa TFF hawataki uchaguzi kwa sababu wanataka kuendelea kubaki madarakani hayana maana hata kidogo.”
Alipoulizwa kuhusu katiba ipi ya TFF itatumika katika mchakato wa uchaguzi huo, Tenga alikataa kutoa ufafanuzi, hali iliyomlazimu Mwenyekiti wa BMT (Dioniz) kuingilia kati na kusema: “Uchaguzi ulisimamishwa na TFF, suala la katiba liko serikalini, nafikiri muulizeni waziri.”
Hata hivyo, ni wazi kwamba katiba ya TFF itakayotumika ni ya 2012 kwa sababu katiba ya 2006 haina vipengele vipya vitatu vya ‘kuondoa nafasi ya makamu wa pili wa rais wa TFF’, ‘usajili wa klabu’ na ‘kuundwa kwa kamati ya rufani ya uchaguzi’ ambayo ni maagizo ya FIFA na makubaliano ya wanachama wa TFF.
Tenga pia aliwataka wagombea wote walioenguliwa na Kamati ya Rufani ya Uchaguzi kujiandaa vizuri, kwani FIFA watakapofika watawasikiliza wao na vyombo vilivyowaengua.
"TFF inaheshimu serikali na itaendelea kufanya hivyo, lakini vilevile lazima iheshimu FIFA kwa sababu iko kwenye mpira wa miguu,” alisema Tenga.
HOJA YA KATIBA
Februari 25, 2013, serikali ilifuta katiba mpya ya TFF ya mwaka 2012 na kutaka itumike ya 2006 kwa maelezo kuwa usajili wake (ya 2012) haukufuata taratibu zilizopo ambazo hukamilika si chini ya siku 14, ikiwa ni pamoja na kujaza fomu namba 6, 7, 8 na 9.
Hoja hiyo ilipingwa na Tenga kwa maelezo kuwa, kama ni kosa lilifanywa na serikali yenyewe kupitia msajili wake na kwamba, hata hiyo katiba ya TFF ya 2006 ilisajiliwa pia kwa utaratibu unaolalamikiwa na serikali.
Hivyo, kwa serikali kukubali mchakato wa uchaguzi uendelee, inamaanisha kuwa agizo la serikali katika hoja hiyo ‘limedunda’ na kwamba, katiba itakayotumika ni ya mwaka 2012.
SIKU 5
Agizo la serikali kuitaka TFF iwe itoe tamko ndani ya siku tano la kukubali kutekeleza maagizo ya kikao baina yao yaliyowataka waitishe mkutano wa katiba ndani ya siku 40 na mkutano mkuu wa uchaguzi kabla ya Mei 25, 2013 halikutekelezwa.
Badala yake, siku moja kabla ya kukamilika kwa muda wa siku tano walizopewa, TFF walitoa barua kutoka FIFA iliyotishia kuifungia Tanzania kama itabainika kuwa serikali inaingilia masuala ya soka.
SIKU 40
Agizo la serikali kwa TFF kutaka mkutano wa mabadiliko ya katiba ufanyike ndani ya siku 40 na mkutano mkuu wa uchaguzi kabla ya Mei 25 pia limegonga mwamba.
Badala yake, Tenga alitoa kauli ya kidiplomasia jana kwa kusema kuwa wako tayari kufanya uchaguzi huo kabla ya Mei 25, lakini hilo litategemea ujio wa ujumbe wa FIFA kusikiliza hoja za walioenguliwa na chombo kilichowaengua.
Kauli hiyo ya Tenga inamaanisha kuwa, kama FIFA watachelewa kuja, serikali haitakuwa na ‘meno’ ya kuilazimisha TFF ifanye mkutano huo wa uchaguzi kabla ya ujio wa FIFA hata kama watakuja Septemba kwani katiba ya TFF haina kipengele chochote kinachoipa serikali mamlaka ya kupanga siku ya uchaguzi.
CHANZO CHA MGOGORO
Chanzo cha mgogoro wa TFF na serikali kilikuwa ni kuenguliwa kwa baadhi ya wagombea wa uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo wakiwamo Michael Wambura anayetaka nafasi ya makamu wa rais na Jamal Malinzi anayewania kumrithi Tenga.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment