ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 25, 2013

Pengo aleta salamu za Papa Francis

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo 

“Wakristo hatuwezi kuinua upanga kuua mtu eti kwa kisingizio kuwa tunatetea Kanisa la Mungu,”alisema Kardinali Pengo, ambaye pia alishiriki katika uchaguzi wa Papa mpya uliofanyika Vatican City.

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameleta ujumbe wa salamu za Papa Francis, ambaye amewataka waumini wake kuukataa ubaguzi wa kidini.

Akizungumza kwenye Ibada ya Matawi iliyofanyika katika Kanisa Katoliki la St Joseph Visiwani Zanzibar jana, Kardinali Pengo alisema Papa Francis amehimiza umoja miongoni mwa wafuasi wa dini zote.

Papa Francis, ambaye ni raia wa Argentina alichaguliwa kuwa Papa wa 266 wa Kanisa Katoliki, Machi 13, mwaka huu akichukua nafasi ya Papa Benedict wa 16 aliyestaafu.

Pengo alisema kuwa ujumbe huo unawagusa Watanzania kwani katika siku za karibuni kumeibuka watu ambao wanadai kuwa wanapigania imani na kwamba wanafanya hivyo kwa kuua watu wengine kinyume na mapenzi ya Mungu.

Alisema vitabu vyote vya dini vinaelekeza kuwa Mungu alimuumba mwanadamu kwa mfano wake, hivyo kitendo cha mwingine kumuua mwenzake kwa kisingizio cha kutetea imani ya dini ni kufuru.

“Wakristo hatuwezi kuinua upanga kuua mtu eti kwa kisingizio kuwa tunatetea Kanisa la Mungu,” alisema Kardinali Pengo, ambaye pia alishiriki katika uchaguzi wa Papa mpya uliofanyika Vatican City.

Kumekuwa na matukio ya viongozi wa dini kushambuliwa katika siku za karibuni hasa Visiwani Zanzibar, akiwamo Padri Evarist Mushi wa Kanisa Katoliki ambaye aliuawa.

Katika tukio lingine Katibu wa Mufti wa Zanzibar, Sheikh Fadhil Soraga alimwagiwa tindikali wakati Padri Ambros Mkenda pia wa Kanisa Katoliki alishambuliwa kwa risasi.

Katika hatua nyingine, Kardinali Pengo alisema uharibifu wa mazingira umeathiri uoto wa asili na ndiyo maana hivi sasa Zanzibar visima ambavyo awali vilikuwa vinatoa majisafi ya kunywa, sasa vinatoa maji yenye chumvi.

Alisema hakuna tena msukumo ambao unayaondoa maji chumvi katika mfumo, ili wapate majisafi ya kunywa jambo ambalo ni la hatari na wanajamii wanapaswa kuliangalia kwa mtazamo wa kipekee badala ya kuwa kama ilivyo sasa.
Mwananchi

No comments: