ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, March 30, 2013

Polisi nchini Kenya waanza kuchunguza kifo cha Mawalla

Arusha. Polisi nchini Kenya kwa kushirikiana na maofisa wa Usalama wa Hospitali ya Nairobi, wameanza uchunguzi juu ya chanzo cha kifo cha wakili maarufu nchini, Nyaga Mawalla kutokana na kuibuka taarifa mpya kuwa hakujiua kwa kujirusha kutoka ghorofani.
Wakizungumza mjini hapa, Mawakili wa Nyaga Mawalla, Arbart Msando na Joseph Nuamannya, walisema hadi jana,  uchunguzi wa kifo hicho ulikuwa  unaendelea na wakakanusha Nyaga kujiua Machi 22, mwaka huu saa 1:30 usiku.
“Tumewaita leo wanahabari kuwaeleza uchunguzi wa kifo cha Wakili Mawalla, unaendelea na tunakanusha taarifa kuwa, Mawalla alijiua kwani, taarifa za kifo chake hazijatolewa na yanayoandikwa na vyombo vya habari mengi ni hisia tu,” alisema Msando.
Msando alisema Polisi Kenya  wanaendesha uchunguzi  kutokana na utata wa kifo hicho, kwani taarifa sasa zinaeleza kuwa Mawalla alipata mauti baada ya kuanguka akiwa ghorofa ya kwanza ya hospitali hiyo.
“Ni kweli kuna taarifa nyingi hizi za kuuawa kabla ya kutupwa chini, au kujiua lakini ukweli haujajulikana na polisi wanachunguza,” alisema Msando.
Kuhusu mazishi, Wakili Msando alisema majadiliano yanaendelea kwani marehemu Nyaga,  aliandika wasia tangu mwaka 2010 kuwa,  akifia nchini azikwe shambani kwake Momella, wilayani Arumeru na akifia nje ya nchi azikwe hukohuko. “Tunachoweza kusema sasa majadiliano yanaendelea na msingi wetu ni wasia wa Nyaga, ambao alikabidhiwa Wakili Fatuma Karume na tayari ameukabidhi kwa familia,” alisema Msando.
Hata hivyo, Wakili Msando alisema  hatimaye mazishi ya Mawalla sasa yatafanyikia Nairobi nchini Kenya, wiki ijayo kama wasia wake ulivyoelekeza.
Alisema ndugu, jamaa na marafiki wamekubaliana kuheshimu wasia huo.
Awali, baba wa marehemu ambaye naye ni wakili wa siku nyingi, alikaririwa akishikilia msimamo wa kutaka mwanae azikwe Marangu, Wilaya ya Moshi Vijijini tofauti na wasia wa marehemu.
Katika wasia huo ulioandikwa mwaka 2009 mbele ya Wakili Fatma Karume, marehemu aliacha maelekezo kuwa kama atafia nje ya nchi, azikwe katika nchi aliyofia.
Pia, wasia huo ambao umekuwa gumzo ulielekeza kuwa kama atafia nchini, azikwe shambani kwake la ekari tatu lililopo Momela, Arusha.
“Tumekaa na familia na tumekubaliana kuheshimu wasia wa marehemu, kwa hiyo tutamzika Kenya alikofia… hatujapanga tarehe lakini inaweza kuwa Jumanne au Jumatano wiki ijayo,” alisema.
Wakili Msando alisema baadhi ya ndugu wa marehemu wataondoka kesho kwenda Nairobi kuanza taratibu za mazishi, ikiwamo kununua eneo ambako atazikiwa.
Mdogo wa marehemu, Obre Mawalla alithibitisha ndugu kukubaliana kuheshimu wasia wa marehemu.
Imeandikwa na Mussa Juma, Arusha na Daniel Mjema, Moshi.
Mwananchi

No comments: