Wachezaji wa Toto Africans, wakiwa wamembeba juu kocha wao baada ya kuifunga Simba katika mchezo wa mwisho wa mzunguko wa kwanza kwenye Uwanja wa Taifa. Picha na Michael Matemanga
Dar es Salaam. Mabingwa watetezi, Simba wakiwa wanachechemea wanashuka kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza kuivaa Toto African leo wakati vinara Yanga wakiwa kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro kuivaa Polisi Morogoro katika harakati za kusaka ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba inashuka uwanjani baada ya kufungwa bao 1-0 na Kagera Sugar katika mchezo uliopita na kubaki nafasi ya tatu ikiwa na pointi 34 sawa wa vijana hao wa Kagera ambao leo wataivaa Mtibwa Sugar.
Yanga inayoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 48 itakuwa Uwanja wa Jamhuri, Morogoro ikicheza na Polisi Moro huku Azam FC inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 40 ikipepetana na Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi.
Kocha wa Yanga, Ernie Brandts amesema wataishambulia Polisi Moro kama nyuki kwa lengo la kushinda mchezo huo na kubakiza dakika 270 (Mechi tatu) kabla ya kutawazwa mabingwa wapya wa ligi hiyo.
Iwapo Yanga itashinda mchezo huo itafikisha pointi 51 na kubakiza pointi tisa tu ambazo ni sawa na mechi tatu kabla ya kutwaa ubingwa wa ligi na kukata tiketi ya kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Yanga ikiwa inawaza ushindi na kutwaa ubingwa, wenyeji wao Polisi watakuwa wakihaha kushinda mchezo huo kukimbia balaa la kushuka daraja.
“Binafsi nafikiri mchezo utakuwa mgumu, kila mtu anapaswa kulifahamu hilo,” alisema kocha Brandts. “Kwa upande wetu tumejipanga vya kutosha kukabiliana nao, lakini hatupaswi kuidharau hata kidogo Polisi,” alisisitiza kocha Brandts.
Naye beki wa Polisi Moro, Chacha Marwa amesisitiza kucheza kwa bidii na kijituma kwa lengo la kuitibulia Yanga kileleni.
“Kwa upande wetu tumejiandaa vya kutosha kukabiliana na Yanga,” alisema beki huyo wa zamani wa Moro United, Mtibwa Sugar na Yanga.
Jijini Mwanza, Simba nao watakuwa na kibarua kigumu pia, kwani watakuwa wakicheza na Toto inayosaka kujinasua na janga la kushuka daraja.
Kocha wa Simba, Patrick Liewig alisema anajua matokeo mabaya waliyoyapata kwenye mchezo wao uliopita dhidi ya Kagera Sugar yatawafanya wachezaji wake wacheze kwa presha kubwa.
“Nimewaambia wachezaji kuwa Toto itatupania kwa sababu inasaka pointi tatu muhimu tena ikiwa kwao,
Toto inataka ushindi ili ijaribu kujinasua kwenye nafasi ya kushuka daraja, tutacheza katika kiwango chetu na uwezo wetu na matumaini yangu hatutafanya makosa tuliyoyafanya kwenye mchezo dhidi ya Kagera Sugar,”alisema Liewig.
Pia, Azam FC inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 40 itakuwa kwenye Uwanja wa Mabatini Mlandizi mkoani Pwani kuikabili Ruvu Shooting.
Kocha wa timu hiyo, Stewart Hall amekiri kuwa mchezo huo utakuwa mgumu kulingana na uwezo wa timu zote mbili.
“Ruvu ni moja kati ya timu ngumu kwenye ligi ukiziacha Yanga na Simba. Ni timu inayoundwa na vijana wengi wenye vipaji,”alisema kocha Hall.
Alisema,”Kwa hiyo natarajia kupata ushindani mkali, lakini kwa upande wetu tumejiandaa vya kutosha kuhakikisha tunashinda mchezo huo.”
Mechi nyingine zinazochezwa leo ni Oljoro JKT itakayokuwa mwenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha wakati vibonde African Lyon watakuwa wakisaka pointi tatu mbele ya Coastal Union kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment