Malkia wa Nyuki akisalimiana na wapenzi na wanachama wa Simba juzi jioni wakati alipotembelea tawi la Mpira Pesa kuanzisha mchakato wa upatanishi baina ya kundi hilo na uongozi wa juu wa Simba.
VIiongozi wa matawi ya Simba jijini Dar es Salaam wakifuatilia kwa makini mkutano wa viongozi wa Simba na matawi jijini uliofanyika makao makuu ya Simba mtaa wa Msimbazi jana.
(Picha zote kwa hisani ya Simba SC)
* Wanachama, uongozi damudamu
* Poppe aombwa kubadili maamuzi yake
* Coastal kuonja 'kisu' cha kwanza leo
* Mazungumzo na Mpira Pesa yanoga
Na Mwandishi Wetu
HALI ya hewa iliyokuwa imechafuka katika klabu ya Simba sasa imerejea katika hali ya kawaida kufuatia Mkutano uliofanyika leo (Machi 9, 2013) baina ya uongozi wa klabu na viongozi wa matawi ya Simba jijini Dar es Salaam katika makao makuu ya klabu hiyo.
Mkutano huo uliitishwa kufuatia hatua ya Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe, kujiuzulu nafasi zao hizo ndani ya klabu siku tatu zilizopita.
Mkutano huo uliongozwa na Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang'are, na kuhudhuriwa na Wenyeviti na Makatibu wa Matawi yote ya klabu jijini Dar es Salaam.
Itang'are, maarufu kwa jina la Mzee Kinesi, alitumia mkutano huo kueleza wanachama mwenendo wa timu katika mashindano tofauti ambayo timu inashiriki na pia hatua zinazochukuliwa kunusuru hali ya sasa.
"Napenda kutumia nafasi hii kuwaomba wanachama wote wa Simba kuendeleza utulivu na mshikamano ndani ya klabu ili tuwe kitu kimoja. Tukiwa kitu kimoja tutaweza kutatua matatizo yetu kwa ufanisi. Tukigawanyika tutazidi kuharibikiwa," alisema.
Katika mkutano huo, viongozi wa matawi waliahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa uongozi ili kuhakikisha Simba inashinda mechi zake zote zilizosalia katika Ligi Kuu ya Tanzania ili iweze kupata miongoni mwa nafasi za juu katika michuano hiyo.
Viongozi hao pia walipendekeza kuundwa kwa jopo la watu wanaoheshimika ndani ya klabu kwa lengo la kwenda kumshawishi Poppe abadili maamuzi yake. Jopo hilo limetakiwa kuanza kazi mara moja ingawa majina ya wanaounda jopo hilo yatafahamika baadaye.
Katika kuhimiza mshikamano ndani ya klabu, juzi jioni Mwenyekiti wa Kamati ya Ushindi Simba, Rahma Al Kharusi, akifuatana na wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, walikwenda kwenye Ofisi za Kundi la Mpira Pesa Magomeni Mikumi jijini Dar es Salaam kuanza mchakato wa upatanishi.
Kundi hilo kwa sasa limesimamishwa na uongozi kutokana na tofauti zilizojitokeza huko nyuma, na Malkia wa Nyuki alisema kamati yake haiwezi kufanya kazi vizuri iwapo kuna migogoro ya ndani kwa ndani baina ya wanachama.
"Nimekuja kwenu leo ili tuzungumze. Lengo hapa ni kutafuta suluhu kwa faida ya Simba. Tukigombana wenyewe kwa wenyewe wanaofaidi ni maadui zetu. Tukae chini, tuzungumze na mwisho wa siku tufikie makubaliano kwa faida ya kklabu yetu," alisema Al Kharusi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mpira Pesa, Ustaadh Masoud, alisema wao hawana nia mbaya dhidi ya Simba isipokuwa kuna mambo ambayo ni lazima yawekwe sawa kwa lengo la kuondoa tofauti zozote zilizokuwapo huko nyuma.
Simba leo inacheza mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania dhidi ya Coastal Union kutoka Tanga na matawi yote yameahidi kushiriki kufanikisha ushindi katika mechi hiyo.
No comments:
Post a Comment