Rais Mstaafu wa Awamu ya tatu,Benjamin Mkapa
Hatua hiyo inalenga katika kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa sekta ya afya huko vijijini.
Arusha. Taasisi ya Mkapa Foundation, inatarajia kujenga nyumba 700 za watumishi wa afya wanaotoa huduma katika maeneo ya vijijini.
Hatua hiyo inalenga katika, kuwaboreshea mazingira mazuri watumishi hao ili waweze kutoa huduma kwa ufanisi.
Hayo yalibainishwa juzi na Ofisa Mipango wa Kitengo cha Uwezeshaji katika taasisi hiyo, Pamela Maro, alipokuwa akizungumzia shughuli zinazofanywa na taasisi hiyo katika kuboresha huduma za afya vijijini.
Alisema lengo la ujenzi wa nyumba hizo ni kuboresha huduma kwa wananchi wa vijijini wanaokabiliwa na changamoto nyingi.
Maro alisema taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kuhakikisha kuwa changamoto zinazowakabili wananchi wao vijijini zinatatuliwa.
Alisema mbali na kujenga nyumba hizo taasisi hiyo pia imekuwa ikiisaidia Serikali kwa kuipatia watumishi wa afya na kuwapeleka katika maeneo ya vijijini.
Alisema tayari taasisi imeshaisaidia Serikali watumishi 230 wa sekta hiyo ambao wamepelekwa katika vituo mbalimbali vya afya na hospitali za wilaya.
Ofisa huyo alisema katika kuhakikisha kuwa huduma zinaboreka zaidi, taasisi imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali kwa timu za wasimamizi wa afya walioko wilayani.
Maro alisema mafunzo hayo pia yametolewa kwa wasimamizi wa vituo vya afya katika mikoa mbalimbali.
Alisema pamoja na jitihada hizo, lakini tatizo la uhaba wa watumishi katika vituo na hospitali mbalimbali ni kubwa sana.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment