ANGALIA LIVE NEWS

Monday, March 11, 2013

Uchaguzi Mkuu Kenya: Ghasia zaanza Kisumu

Nairobi: Polisi wa kutuliza ghasia juzi walilazimika kutumia mabomu ya machozi Mjini Kisumu kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakipinga kutangazwa kwa matokeo ya urais ambayo mgombea wao, Raila Odinga alianguka.
Vurugu hizo ziliibuka, baada ya kutangazwa kwa matokeo ya urais yaliyompa ushindi Uhuru Kenyatta.
Maelfu ya vijana wamekuwa wakirandaranda kwenye maeneo kadhaa ya Kisumu wakichoma majengo na kufunga barabara, huku wakiimba: “Bila Raila, hakuna amani.”
Vurugu hizo zilizoanza juzi jioni zimesababisha maduka kufungwa huku makundi ya vijana wenye hasira wakiendelea kurandaranda mitaani wakipambana na polisi ambao walifanya jitihada za kuwatuliza na kurejesha amani.
Ilielezwa kwamba, muda mfupi tu baada ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kumtangaza Kenyatta kuwa mshindi, zaidi ya vijana 100 waliibuka na kuanza kuwarushia mawe polisi na muda mfupi baadaye idadi ya vijana hao iliongezeka na kusambaa katika maeneo karibu yote ya Kisumu.
Odinga ambaye alikuwa mgombea wa Muungano wa Cord, amewataka wafuasi wake kuwa watulivu kwa kuwa anahitaji kufuata mkondo wa sheria kupinga matokeo hayo.
Matokeo hayo yaliyotangazwa juzi, yalimpa ushindi Kenyatta aliyesimama kwa tiketi ya Muungano wa Jubilee, wa asilimia 50.07 dhidi ya asilimia 43 alizopata Raila.
Raila atinga mahakamani
Muungano wa Cord, leo utawasilisha vielelezo mahakamani kupinga ushindi wa Kenyatta.
Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Kenya, Amos Wako ametajwa kuwa miongoni mwa wajumbe wa jopo la wanasheria watakaopinga ushindi wa Kenyatta.
Jopo hilo la wanasheria linaongozwa na mwanasheria mkongwe, George Oraro na baadhi ya mawaziri wakiwamo; Mutula Kilonzo, James Orengo na Ababu Namwamba ambao ni washauri wakuu wa jopo.
Oraro alimtetea aliyekuwa Waziri wa Viwanda, Henry Kosgei wakati alipokabiliwa na kesi kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICC, The Hague.
Wengine wanaounda timu hiyo ni Gitobu Imanyara, Pheroze Nowrojee, Chacha Odera, Ambrose Rachier na Paul Mwangi.
Cord imepanga kufungua kesi ikitaka Mahakama itengue hatua ya kutangazwa kwa Kenyatta kuwa Rais wa Kenya kwa kuwa taratibu za ukusanyaji matokeo zilikiukwa.
Tangu juzi, jopo hilo la wanasheria lilikuwa na vikao mfululizo kuandaa ushahidi wa kesi hiyo ikiwamo kukusanya vielelezo watakavyosimamia katika kesi hiyo kwa mujibu wa Kifungu namba 163 cha Katiba ya Kenya.
Mfuasi wa Uhuru afariki
Shamrashamra za kushangilia ushindi wa Kenyatta ziliingia doa kwenye Mji wa Nyeri baada ya lori lililobeba mashabiki wa mgombea huyo kutumbukia kwenye korongo na kuua mtu mmoja. Katika ajali hiyo watu 30 walijeruhiwa lakini wakiwa katika hali mbaya.
Mwili wa mtu aliyefariki ulipelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Nyeri wakati wengine waliojeruhiwa wamelazwa kwenye hospitali hiyo.
Lori hilo lilikuwa likienda maeneo ya Giakanja kwa ajili ya kukusanya mashabiki wengine na kuanza safari ya kuzunguka mitaa ya mji huo kushangilia ushindi. Kamanda wa Polisi Nyeri, Kirunya Limbitu alithibitisha ajali hiyo na kusema lori hilo lilikuwa kwenye mwendokasi na kupoteza mwelekeo kabla ya kutumbukia kwenye korongo na kupinduka.
Mwananchi


No comments: