ANGALIA LIVE NEWS

Friday, March 8, 2013

Vigogo wavuliwa madaraka TBS

Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS), imewavua madaraka wakurugenzi wawili.
Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Profesa Cuthbert Mhilu alisema jana kuwa waliovuliwa madaraka ni aliyekuwa Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora, Dominic Mwakangale na aliyekuwa Mkurugenzi wa Upimaji na Huduma za Vifungashio, Kezia Mbwambo.
Profesa Mhilu alisema hatua hiyo imekuja baada ya bodi hiyo kufanya usaili kwa vigogo mbalimbali wa shirika hilo ulioanza juzi asubuhi hadi saa 3:00 usiku.
Katika taarifa hiyo, Profesa Mhilu ambaye hakutaka kuingia kwa ndani juu ya hatua hiyo, alisema viongozi hao watapangiwa kazi nyingine.
“Kwa kipindi kirefu, TBS imekuwa ikikabiliwa na matatizo mbalimbali yaliyochangia kudhoofisha utendaji wa watumishi na kulifanya shirika kukosa tija na ufanisi. Bodi imeonelea ikae mara moja kuchambua, kujadili na hatimaye kufikia uamuzi wenye lengo la kuweka mazingira bora na kuwezesha kuanza utatuzi wa matatizo ili shirika lifikie malengo yake.”
Baada ya hatua hiyo, bodi hiyo ilimteua Tumaini Mtitu kuwa Mkurugenzi mpya wa Udhibiti Ubora na Agnes Mneney kuwa Mkurugenzi wa Upimaji na Huduma za Vifungashio.
Wengine walioteuliwa ni Emmanuel Ntelya atakayekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Shirika na Edna Ndumbaro kuwa Meneja Uandaaji Viwango vya Uhandisi.
Kadhalika, Matrida Kasanga ameteuliwa kuwa Meneja wa Hati na Tehama na Anitha Kaveva anakuwa Meneja Mipango na Utawala.
Alipoulizwa kama hatua hiyo inakwenda sanjari na sifa baada ya kufanyika kwa usaili Profesa Mhilu alisema: “Ninachowaambia ni hicho... hakuna tatizo tulilobaini kuhusu viongozi hawa, haya ni mabadiliko ya kawaida.”
Alipoulizwa kuhusu hatua hiyo, Mbwambo alijibu kwa kifupi: “Sifahamu, wasiliana na mwenyekiti wa bodi au  mkurugenzi mkuu ndiyo wenye nafasi ya kuzungumzia zaidi kuhusu hatua hiyo.”
Mwalangale hakupatikana na hata alipotafutwa kwa simu yake ya mkononi iliita bila ya kupokewa.
Akizungumzia uteuzi huo, Profesa Mhilu alisema: “Hata hawa tuliowateua kushika nyadhifa hizo watambue kwamba tutawafuatilia kwa karibu tukiangalia utendaji wao, asiyefanya kazi kwa ufanisi atang’olewa.”
Alisema Bodi hiyo imetoa maagizo kwa Menejimenti ya TBS kuhakikisha kwamba inakomesha bidhaa feki, inafanya ukaguzi wa magari, pia kuhakikisha inaondoa urasimu wa upatikanaji wa leseni kwa wajasiriamali wadogo lakini kwa kuzingatia viwango vya bidhaa wanazotengeneza.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Joseph Masikitiko alisema kuwa amejipanga kushirikiana na menejimenti yake ikiwa ni pamoja na kukomesha makundi miongoni mwa wafanyakazi ili kuleta tija.
Tangu ilipozinduliwa, bodi hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa ya kusafisha safu za utawala za shirika hilo baada ya kuanza kwa kumvua madaraka Kaimu Mkurugenzi Mkuu Leandiri Kinabo na kumteua Masikitiko kabla ya kuitisha usaili upya wa wakurugenzi.
Mwananchi

No comments: