Watoto wa watawala wa kwanza wa Nchi ya Kenya, Rais Jomo Kenyatta na Makamu wake wa Kwanza wa Rais Jaramogi Odinga Odinga wanazidi kuchuana vikali kuwania kiti cha Urais Kenya huku Kenyatta akiwa mbele kwa tofauti ya kura zaidi ya 1,036,834.
Matokeo ya Uchaguzi nchini Kenya hadi kufikia Usiku wa Machi nane saa 3:45 yalionesha kuwa Uhuru Kenyata alikuwa mbele kwa kura 5, 824,901 dhidi ya kura 4,788,067 za Mgombea wa ODM, Raila Odinga.
Hadi kufikia muda huo ni kura 11,359,686 ndio zilikuwa zimekwisha hesabiwa kutoka katika majimbo 264 kati ya majimbo 291 ya Uchaguzi.
Aidha katika kura hizo kura 100,567 zimeharibika hivyo kufanya kura halali hadi sasa kufikia 11,251.
Katika kinyang’anyiro hicho Wycliffe Musalia Mudavadi anashika nafasi ya tatu akiwa amejikusanyia kura 431,056 a nafasi ya nne ikienda kwa Peter Kenneth mwenye kura66,999.
Mgombea wa Alliance for Real Change,Mohamud Abduba Dida anashika nafasi ya tano akiwa na kura 51,093 akifuatiwa na Mwana mama Martha Karua wa National Rainbow Coalition mwenye kura 40,309 hadi sasa.
Nafasi ya saba katika wagombea hao Urais inakwenda kwa James ole Kiyiapi wa Chama cha Restore and Build Kenya ambaye ana kura 36, 317 huku nafasi ya ya nane na mwisho ikishikwa na Paul Kibugi Muite wa chama cha Safina.
WAJUE WAGOMBEA URAIS NCHINI KENYA 2013
Raila Amollo Odinga
Waziri Mkuu Raila Amollo Odinga alizaliwa Januari 7, 1945 huko Maseno, Nyanza, mtoto wa Makamu wa Rais wa kwanza Jaramogi Oginga Odinga. Anagombea kupitia kupitia ushirika wa CORD na Makamu Rais Kalonzo Musyoka akiwa mgombea mwenza wake. Odinga ametilia mkazo maswala ya vijana katika kampeni yake, akiahidi kuwasaidia kuwapatia kazi zaidi na elimu. Odinga alijihusisha katika siasa za upinzani kwa miaka mingi kabla ya kuteuliwa Waziri Mkuu katika muafaka uliofuatia ghasia za uchaguzi wa mwaka 2007.
Uhuru Muigai Kenyatta
Uhuru Muigai Kenyatta alizaliwa Octoba 1961. Baba yake ni rais wa kwanza wa Kenya Jomo Kenyatta, ambaye aliongoza Kenya kutoka 1964 mpaka 1978. Anawania urais kama mgombea wa Jubilee Alliance, ulioundwa kwa ushirikiano wa chama cha The National Alliance cha Kenyatta na United Republican cha William Ruto. Katika ushirika wao, Kenyatta anasema anasimamia Kenya iliyoungana chini ya “ndoto moja ya kujenga Kenya bora”. Aliwania urais 2007, lakini baadaye akamwunga mkono Rais Mwai Kibaki. Kibaki alimchagua Kenyatta kama waziri wa serikali za mitaa Januari 2008 kabla ya kuwa naibu makamu waziri mkuu na waziri fedha mwaka 2008 kama sehemu ya mapatano ya serikali ya ushirika kumliza ghasia za baada ya uchaguzi za mwaka 2007.
Mohamud Abduba Dida
Mohamud Abduba Dida alizaliwa katika wilaya ya Wajir mwaka 1975. Mwalimu wa zamani, Dida anagombania urais kupitia Alliance for Real Change. Mgombea wake mwenza ni Joshua Odongo Onono, pia mwalimu wa zamani. Dida, mwanasiasa mpya, ameahidi kutilia mkazo masikini kama rais. Anasema elimu ni budi iwe bure kwa Wakenya. Alisifiwa kwa kufanya vizuri sana katika midahalo yote miwili ya urais iliyofanyika kwa mara ya kwanza Kenya katika matayarisho ya uchaguzi.
Martha Karua
Martha Karua, mgombea pekee mwanamke katika uchaguzi huu, alizaliwa Septemba 1957 huko Kirinyaga, Central Province. Karua, mbunge wa Gichugu, anagombania kupitia ushirika wa National Rainbow Coalition akifuatana na mbunge wa zamani wa bunge la Afrika Mashariki, Augustine Lotodo. Karua ameahidi kuwakilisha Kenya iliyoungana na maswala ya mageuzi ya uchumi nay a kijamii, ikiwa ni pamoja na afya kwa wote. Anasema atatumia asilimia 10 ya bajeti ya Kenya kuboresha uzalishaji katika kilimo, kuongeza uzalishaji nishati na kuhakikisha asilimia 50 ya nyumba za Kenya zinapata huduma wa mtandao katika muda wa miaka mitano.
Peter Kenneth
Peter Kenneth
Peter Kenneth alizaliwa Novemba 1965 Bahati, Nairobi. Ni mbunge ambaye anajulikana kwa uhodari katika maswala ya fedha na benki. Anawania urais kupitia chama cha Kenya National Congress, na mgombea mwenza wake ni Ronald Osumba, meneja wa zamani katika kampuni ya simu ya Safaricom. Kama mgombea, Kenneth ametilia mkazo kupunguza ukosefu wa kazi na kukosekana kwa chakula. Kutoka mwaka 2003 mpaka 2005, alikuwa waziri mdogo katika wizara ya Maendeleo na Masoko, na baadaye kama waziri mdogo katika Wizara ya Fedha mpaka 2007. Tangu mwaka 2008, amekuwa waziri mdogo katika Wizara ya Mipango, Maendeleo ya Taifa na Dira ya 2030.
James ole Kiyiapi
James ole Kiyiapi alizaliwa Mei 1961 huko Osupuko, Rift Valley Province. Alifanya kazi kama katibu mkuu katika wizara mbali mbali kabla ya kujiuzulu mwaka 2012, anafuatana na mfanyabiashara Winnie Kaburu kama mgombea mwenza chini ya chama cha Restore and Build Kenya. Kiyiapi anagombania kwa nguvu ya swala la kuondoa ukabila katika siasa za Kenya. Anasema kipaumbele chake cha kwanza kama akichaguliwa itakuwa kutilia mkazo vijana na ukosefu wa kazi. Anasema serikali yake itaanzisha mpango wa kupata ufumbuzi wa matatizo ya ardhi kwa uangalifu na uwazi, na kuboresha uzalishaji kilimo nchini.
Wycliffe Musalia Mudavadi
Naibu Waziri Mkuu Wycliffe Musalia Mudavadi alizaliwa September 1960 huko Sabatia, Western Province. Anagombania chini ya chama cha United Democratic Forum Party katika ushirika wa Amani alliance, na Jeremiah Kioni, mbunge kutoka Ndaragwa. Mudavadi ameahidi kuleta ukuaji wa kweli wa uchumi Kenya kwa kutilia mkazi utawala bora na kupunguza umasikini. Mudavadi alikuwa mbunge mwaka 1989, alipochaguliwa bilwa kupingwa kuchukua nafasi ya marehemu baba yake Moses Mudavadi, katika jimbo la Sabatia.
Paul Kibugi Muite
Paul Kibugi Muite alizaliwa Aprili 1945. Ni mbunge wa zamani kutoka jimbo la Kabete ambaye pia ni mmoja wa waanzilisha wa chama cha Safina. Anashirikiana na Shem Ochuodho, waziri wa zamani wa nishati na mbunge wa Rangwe. Muite anasema akiwa rais atashughulikia swala la ukosefu wa kazi na kuboresha hali ya utendaji kazi kwa kuongeza mishahara nja kutekeleza sheria za kazi ambazo zitaweka kiwango cha masaa ya kazi kuwa manane pekee kwa siku. Anasema anaamini umoja wa wananchi wa Kenya, bila kujali ukabia, na atashughulika kuboresha hali ya watu wote. Muite, ambaye ni mwanasheria wa haki za binadamu, alikuwa miongoni mwa viongozi mashuhuri walioshinikiza kumaliza kwa siasa za chama kimoja katika miaka ya 1990.
Habari kwa hisani ya Father Kidevu Blog
No comments:
Post a Comment