ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 9, 2013

Balaa jipya

  Wajumbe wa NEC watano waitwa kuhojiwa
  Wote wanatoka UVCCM, Mwenyekiti ndani
Mwenyekiti wa UVCCM, Hamisi Juma Sadifa .
Sasa ni dhahiri vita ya kusaka nani aliingia madarakani kwenye uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) imeanza kuchukua sura mpya baada ya kuwapo habari kwamba vigogo watano wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), wameitwa kuhojiwa na Kamati ya Maadili ya chama hicho leo.

Habari kutoka ndani ya chama hicho, zinasema kuwa, miongoni mwa wanaotakiwa kuhojiwa ni pamoja na Mwenyekiti wa UVCCM, Hamisi Juma Sadifa na Makamu wake, Mboni Mhita.

Wengine ni wajumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) kupitia vijana, Deogratias Ndejembi, Jonas Nkya na Jerry Silaa, ambaye pia ni Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, Jijini Dar es Salaam na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho.
Baadhi ya vigogo wa UVCCM waliohojiwa na NIPASHE jana, wamethibitisha kupokea ujumbe wa kuitwa kwenda kuhojiwa na kamati hiyo.

Miongoni mwa vigogo waliothibitisha suala hilo, ni pamoja na Mwenyekiti Sadifa na Nkya, lakini wote kwa nyakati tofauti hawakuwa tayari kuzungumzia kwa undani suala hilo kwa kuwa kanuni haziwaruhusu.

“Wewe nitafute kesho saa 10 jioni nitakuwa katika nafasi nzuri ya kujibu swali lako,” alisema Sadifa akijibu swali la NIPASHE kama atakwenda kwenye kuhojiwa na Kamati ya Maadili saa ngapi.

Habari za awali zilidai kwamba, vigogo hao wa UVCCM waliitwa na Ofisi ya Makamu Mwenyekiti wa CCM kwenda kuhojiwa na kwamba walitumiwa ujumbe mfupi wa simu (sms) badala ya barua kama taratibu zinavyotaka.

Alipoulizwa na NIPASHE jana, Nkya alisema “Ni kweli tumeitwa kwenda kuhojiwa kesho (leo).”

Alisema alipokea wito wa kwenda kuhojiwa na kamati hiyo jana.

Nkya alisema wito huo ulitumwa kwake na makatibu muhtasi wa Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Barabara ya Lumumba, jijini Dar es Salaam, kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi (sms).

“Ni kweli tumeitwa. Tumetakiwa kufika kwenye Kamati ya Maadili leo,” alisema Nkya.

Alisema si yeye tu, bali kuna baadhi ya viongozi wa UVCCM ambao hakuwataja, pia wameitwa kwenda kuhojiwa na kamati hiyo leo.

Hata hivyo, alisema hadi jana jioni alikuwa hajui walichoitiwa na kamati hiyo.

“Sijui nini tulichoitiwa. Umekuja ujumbe. Nimepata ujumbe wa sms. Nadhani walioutuma ni masekretari wa makao makuu ya chama,” alisema Nkya.

Vigogo wengine wanaodaiwa kuitwa kwenda kuhojiwa, hawakupatikana jana kuthibitisha suala hilo.

Baadhi walipopigiwa simu zao mikononi, ziliita bila kupokelewa na wengine hadi tunakwenda mitamboni simu zao zilikuwa zimezimwa.

Ingawa hakuna aliyekuwa radhi kusema kwa undani wito huo unalenga nini, habari za ndani ya CCM zinasema kuwa kinachoendelea ni kusaka mchawi kwa kisingizio cha rushwa.

Vijana hao wanadaiwa kuwa walishinda nafasi zao za sasa kwa njia ya rushwa.

Itakumbukwa kwamba Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Philip Mangula, baada ya uchaguzi mkuu wa CCM mwaka jana, alisema kuwa watawasaka wote walioshinda nafasi mbalimbali ndani ya chama hicho kwa njia za rushwa. Alitoa miezi sita kwa kazi hiyo kukamilika.

Hata hivyo, jana Mangula alipoulizwa na NIPASHE alisema hana anachojua kuhusiana na sakata hilo la vigogo wa UVCCM.

“Mimi kama mnavyojua nipo huku kijijini kwangu na kimwana wangu Njombe honeymoon (fungate). Hayo ya vijana unayoniuliza mimi siyajui,” alisema Mangula.

Kwa mujibu wa habari hizo, hatua ya kuhojiwa kwa vigogo hao wa UVCCM, inafuatia kuzuka kwa mvutano mkubwa miongoni mwa vijana katika umoja huo.

Mvutano huo unadaiwa kumhusisha kigogo mmoja wa UVCCM na mtoto wa kigogo serikalini.

Inadaiwa kuwa mvutano huo unatokana na mtoto huyo wa kigogo pamoja na baadhi ya wanachama wa UVCCM wanaomuunga mkono kupinga mabadiliko yanayodaiwa kufanywa na kigogo huyo wa umoja huo.

Mabadiliko hayo yanayodaiwa kufanywa na kigogo huyo wa UVCCM yametajwa kuwa ni pamoja na kuwaondoa baadhi ya wakuu wa idara katika nafasi zao makamu makuu ya jumuiya.

Mabadiliko hayo yanadaiwa kuwa yamekuwa yakilalamikiwa vikali na mtoto huyo wa kigogo serikalini kwa madai kuwa anahujumuiwa.

Mtoto huyo wa kigogo anadaiwa kuwa mabadiliko hayo yanamuumiza kwa kuwa yamekuwa yakifanywa na kigogo huyo wa UVCCM, kwa kuwalenga wanachama wanaomuunga mkono.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

CCM iweni makini ,iweni wakweli