Kumekuwa na kitendawili cha juu ya nani hasa anayetuhumiwa kuhusika na kutekwa na kuteswa kwa Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa New Habari (2006) Limited wachapishaji wa magazeti ya Rai, Dimba, Mtanzania, Bingwa na The African, kulikofanywa na watu ambao hadi saa bado hawajafahamika.
Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Isaya Mngulu, alisema jana kuwa, ripoti ya upelelezi wa timu maalum ya wapelelezi itatolewa kati ya Aprili 15, 16 au 17, mwaka huu.
Mngulu alisema hayo alipokuwa akihojiwa jana asubuhi na kipindi cha ‘Kumepambazuka’, kinachorushwa hewani na Radio One Stereo.
Alisema ripoti hiyo ndiyo itakayobainisha kama kuna watu wanaostahili kushtakiwa mahakamani kwa tuhuma za kuhusika na sakata hilo au la.
“Hapo ndipo itakapojulikana kama kuna washtakiwa au hakuna washtakiwa,” alisema Mngulu.
Alisema miongoni mwa watu waliohojiwa katika upelelezi uliofanywa na timu hiyo, ni pamoja na Kibanda mwenyewe.
Akijibu swali kwa nini upelelezi wa sakata hilo umechukua muda mrefu, Mngulu alisema hakuna muda maalum uliowekwa na sheria wa kupeleleza jambo.
Kutokana na hali hiyo, alisema upelelezi unaweza kuchukua hata miaka 10 na zaidi.
Mngulu ambaye alizungumza kwa ufundi na kwa tahadhari kubwa katika mahojiano hayo, alisema hata katika kumsaka Osama bin Laden ilichukua zaidi ya miaka 10 ndipo akanaswa.
Alisema sheria, kanuni na taratibu za upelelezi haziruhusu kueleza mwenendo, mbinu na maendeleo ya upelelezi wakati kazi hiyo inapokuwa inafanyika.
Hivyo, akawataka Watanzania kuwa wastahamilivu na wenye subira hadi upelelezi huo utakapokamilika na ripoti hiyo kutolewa.
Kibanda alivamiwa na watu hao, wakati akirejea nyumbani kwake, Mbezi Juu, jijini Dar es Salaam Machi 5, mwaka huu.
Katika tukio hilo, watu hao walimng’oa meno, kucha na kumharibu jicho la kushoto.
Hali hiyo ilisababisha Kibanda kulazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), baadaye katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), jijini Dar es Salaam kabla ya kuhamishiwa Afrika Kusini ambako anaendelea na matibabu zaidi.
Kufuatia tukio hilo, Msemaji Mkuu wa Jeshi la Polisi, Advera Nsenso, alikaririwa akisema Mkuu wa Jeshi hilo nchini, Inspekta Jenerali (IGP), Said Mwema, ameunda timu ya wapelelezi wazoefu kufanya uchunguzi wa kimaabara ili kuwabaini waliohusika na uhalifu huo na kuwatia mbaroni mara moja.
Timu hiyo ya makachero wanne kutoka makao makuu ya polisi iliunganisha nguvu na makachero wa Jeshi hilo Kanda Maalum ya Dar es Salaam.
Hadi kufikia jana, hakukuwa na taarifa zozote za kukamatwa mtu kuhusiana na tukio hilo.
Habari ambazo NIPASHE inazo, kigogo mmoja wa polisi alikwenda Afrika Kusini kumhoji Kibanda ikiwa ni pamoja na kuchukua maelezo yake juu ya mkasa mzima wa kufanyiwa unyama wa kutisha unaofanana na ule aliofanyiwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Stephen Ulimboka.
Ingawa Polisi hawataki kusema kama wamekamata yeyote hadi sasa, kuna uvumi kuwa kuna watu kadhaa wamekamatwa kutoka maeneo mbalimbali, akiwamo mmoja aliyekamatwa mkoani Kagera kuhusiana na tukuo hili.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment