ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 8, 2013

Balozi Seif Ali Iddi asisitiza umuhimu wa Wafanyabiashara Nchini kuzingatia suala la Bima

Mkuu wa Makontena yaliyoungua moto Darajani Bwana Suleiman Masoud akimuelezea Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif usumbufu wanaoupata kutokana na ufinyu wa maeneo ya kufanyia baiashara zao. Kushoto yao ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohd Aboud Mohd.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiwa na Waziri wake Mh. Mohd Aboud Mohd wakifika eneo la Darajani katika maduka yaliyoungua moto kuwafariji wafanyabiashara waliopatwa na ajali hito.
Balozi Seif akiangalia bidhaa katika maduka ya jirani nay ale yaliyoungua moto ambapo wamiliki wake walilazimika kuondosha bidhaa zao wakati wa maafa hayo ya mato.
Juu na chini ni baadhi ya Bidhaa zilizoungua moto katika Duka la Bwana Abdulla Hemed Khamis liliopo Darajani Mjini Zanzibar pembezoni mwa eneo la maduka linalomilikiwa na Chama cha Mapinduzi Afisi Kuu Kisiwandui.


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amesisitiza umuhimu wa Wafanyabiashara Nchini  kuzingatia suala la Bima katika kuendesha Biashara zao ili kujijengea umakini wakati wanapopatwa na majanga.
Sisitizo hilo amelitoa mara baada ya kukagua maduka mawili yaliyoungua moto kutokana na hitilafu ya umeme  pembezoni mwa eneo la maduka linalomilikiwa na Chama cha Mapinduzi CCM hapo Kisiwandui Mjini Zanzibar.
Balozi Seif alisema wafanyabiasha wengi wamekuwa wakishindwa kuendelea na biashara zao  wakati wanapopatwa na majanga mbali mbali na kushindwa kurejesha mtaji huo kutokana na kukosa  Bima.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisema faraja kubwa hupatikana kwa washirika wa Bima na hii faida yake huonekana pale muhusika anapokumbwa na majanga ndani ya harakati zake za kibiashara.
“ Sijui kwa nini wafanya biashara wetu wamekuwa wagumu katika kukata bima ambayo msingi wake hauonekani ghafla pale mfanyabiashara anapokutwa na balaa ya Maafa katika bishara yake”. Alisisitiza BaloziSeif.
Balozi Seif aliwapa pole wafanyabiashara hao na kuwataka kuendelea kuwa na subra wakati huu mgumu wanaoendelea kukabiliana nao kuyokana na ajali hiyo ya moto.
Mapema Mmoja wa Wafanyabiashara walioathirika na ajali hiyo Bwana Abdulla Hemed Khamis alimueleza Balozi Seif kwamba chanzo cha moto huo kinatokana na hitilafu ya umeme iliyosababishwa na wezi waliowahi kuiba baadhi ya bidhaa za chakula siku mbili zilizopita.
“ Mimi nilifika muda mfupi kwenye duka langu baada ya kupata taarifa wakati tayari nilikuwa nimeshaondoka eneo hilo. Lakini nakishukuru kikosi cha Zima moto na Uokozi Zanzibar kilichosaidia kuuzima moto huo katika kipindi kifupi sana”. Alieleza Bwana Hemd.
Bwana Hemed alisema eneo lao la biashara limekuwa  likikumbwa na wizi wa mara kwa mara unapelekea kuwavunja moyo katika harakati zao za kujitafutia riziki kupitia sekta hiyo ya biashara.
Hata hivyo Mfanyabiashara huyo wa biashara ya vyakula mchanganyiko bwana Abdulla Hemed Khamis alishindwa kukisia hasara halisi iliyompata kutokana na moto huo.
Naye kwa upande wake Mkuu wa Makontena hayo Bwana Suleiman Masuod aliiomba Serikali kushajiisha  Wawekezaji  kufikiria kujenga majengo makubwa ya Biashara { Shooping Mole } kwa lengo la kuwaondolea usumbufu wafanyabiashara wa ngazi ya kati.
Bwana Suleiman alimueleza Balozi Seif kwamba majengo hayo yanastawisha maeneo ya mji na kutoa haiba inayovutia kwa vile majengo la makontena hayatoi sura nzuri.
 Taarifa kwa hisani ya Salma Said
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

No comments: