Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiagana na mkuu wa program za “sober houses Zanzibar”, Suleiman Mauly, baada ya kufungua kampeni ya kupunguza dawa za kulevya maskulini, hafla iliyofanyika skuli ya Lumumba. Katikati ni Mkurugenzi mkaazi wa kampuni ya “Double Tree Tanzania” bw. Judd Lehmann.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa taasisi za mapambano dhidi ya dawa kulevya pamoja na wanafunzi baada ya kufungua kampeni ya kupunguza dawa za kulevya maskulini, hafla iliyofanyika skuli ya Lumumba.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa taasisi za mapambano dhidi ya dawa kulevya pamoja na vijana walioacha matumizi ya dawa hizo, baada ya kufungua kampeni ya kupunguza dawa za kulevya maskulini, hafla iliyofanyika skuli ya Lumumba.
Mkurugenzi mkaazi wa kampuni ya “Double Tree Tanzania” bw. Judd Lehmann akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa kampeni ya kupunguza dawa za kulevya huko skuli ya Lumumba.
Taarifa na picha kwa hisani ya Salma Said
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad amesema Serikali italazimika kuchukua hatua za dharura katika kukabiliana na wafanyabiashara wa dawa za kulevya nchini.
Amesema wafanyabiashara hao wamekuwa wakiwatumia vijana kwa ajili ya kununua na kusambaza dawa za kulevya, bila ya kuzingatia athari zitokanazo na biashara hiyo haramu ambayo pia huzorotesha maendeleo ya kiuchumi kwa taifa.
Maalim Seif ameeleza hayo leo katika hafla ya ufunguzi wa kampeni ya kupunguza matumizi ya dawa za kulevya na athari zake maskulini, iliyofanyika skuli ya sekondari ya Lumumba.
Amesema ni lazima zitumike hatua za dharura katika kuwashughulikia wafanyabiashara hao, vyenginevyo taifa litaendelea kuangamia kutokana na matumizi makubwa ya dawa za kulevya.
Amefahamisha kuwa wafanyabiashara wa dawa za kulevya wamekuwa wakijali zaidi maslahi yao, na kuamua kuwatumia vijana kuendeleza biashara na matumizi ya dawa hizo, jambo ambalo halikubaliki kwa mustakbali wa Zanzibar.
Amewatahadharisha vijana kuwa makini na wafanyabiashara hao na kutokubali kutumiwa katika biashara hiyo.
Ufunguzi wa kampeni hiyo iliyoandaliwa na “Sober Houses” chini ya ufadhili ya Hoteli ya “Double Tree Tanzania”, umekwenda sambamba na uzinduzi wa chapisho maalum la kitabu ambacho kitatumika kufundishia maskulini.
Maalim Seif amefahamisha kuwa kampeni hiyo ni muhimu katika kuwashajiisha wanafunzi na jamii kwa ujumla kutojiingiza katika matumizi ya dawa za kulevya na kufikia lengo la kuwa na Zanzibar isiyokuwa na matumizi ya dawa za kulevya.
Mapema Mkurugenzi mkaazi wa kampuni ya “Double Tree Tanzania” bw. Judd Lehmann amesema kampuni yake ambayo tayari imeshatoa shilingi milioni 24, itaendelea kusaidia maendeleo ya kijamii ikiwa ni pamoja na kusaidia utoaji wa elimu juu ya kukabiliana na matumizi ya dawa za kulevya.
Amefahamisha kuwa kampeni hiyo inaweza kuleta mafanikio makubwa kutokana na uamuzi wa kuipeleka maskulini ambako watumiaji wengi wa dawa hizo wamekuwa wakianzia huko.
Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mkurugenzi wa Elimu ya Maandalizi na Msingi bw. Uledi Juma Wadi amesema mpango wa kutoa elimu kuhusu dawa za kulevya maskulini ni muhimu katika kupambana na janga hilo.
Amesema Wizara ya elimu inazo program nyingi za kuwaelimisha wanafunzi juu ya kukabiliana na majanga mbali mbali, na kwamba itaendelea kushirikiana na Jumuiya zinazolenga kuwaelimisha wanafunzi kwa maendeleo ya taifa.
Nae mkuu wa programu za “Sobber Houses” Zanzibar bw. Suleiman Mauly amesema “sober house” ni pahala salama kwa vijana walioamua kuachana na dawa za kulevya.
Amesema tayari programu hizo zimeshawakomboa vijana wengi kwa kuwapatia matibabu ya ushauri nasaha, na hatimaye kuweza kuwarejesha skuli na vyuoni vikiwemo chuo kikuu huria na chuo cha maendeleo ya utalii.
No comments:
Post a Comment