Advertisements

Wednesday, April 17, 2013

Idara ya Afya kutoa ajira 16,000

Dodoma. Jumla ya watumishi 16,000 wa kada ya afya, wanatarajia kuajiriwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/14 na 2014/15, bunge lilielezwa jana.
Ahadi hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani kuwa ajira hizo zinalenga kupunguza tatizo sugu la watumishi wa kada hiyo ambao wamekuwa wakilalamikiwa.
Akijibu swali la nyongeza jana lililoulizwa na Mbunge wa Lupa, Victor Mwambalaswa (CCM), Kombani alisema kuwa katika kipindi cha mwaka huu Serikali inatarajia kutoa ajira kwa waganga 5,000.
“Mwaka huu pekee tunaanza na waganga 5,000 ambao tayari tumeshapewa kibali cha kuajiri na kipaumbele kikubwa kitaelekezwa katika zahanaiti za vijijni lakini mwaka tutaajiri waganga 11,000, wengi wao kwenda vijijini badala ya kuwalundika mijini,” alisisitiza Kombani.
Awali, katika swali la msingi, Mendrad Kigola (Mufindi Kusini-CCM) alitaka kujua ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa vituo vya afya ambavyo wananchi wamejitolea na kufikia hatua nzuri pamoja na kupelekea waganga.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Aggrey Mwanri alijibu swali hilo akisema kuwa miradi mingi ya ujenzi wa vituo vya afya na zahanati kwa sehemu kubwa huibuliwa na wananchi, hivyo gharama za utekelezaji wa miradi hiyo hutoka kwa wananchi pia.
Mwanri alisema ujenzi wa vituo vya afya vya Mtwango, Mninga, Mgololo na Bumilayinga katika Jimbo la Mufindi, ni miradi ambayo iliibuliwa na wananchi wenyewe na kuwa inatekelezwa na wananchi wenyewe.
Hata hivyo, alisema kuwa Serikali itawaunga mkono wananchi hao kupitia Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi kwa kadri fedha zinatakavyopatikana.
Hakuna shaka kwamba mpango kama huo utasaidia kupunguza tatizo la ajira ambalo linaonekana kusumbua Watanzania wengi.
Hali kadhalika kuajiriwa kwa watu hao wapatao 16,000 kutasaidia kuimarisha sekta hii muhimu ambayo inaonekana kuendelea kusuasua nchini hasa maeneo ya vijijini.     

No comments: