ANGALIA LIVE NEWS
Wednesday, April 17, 2013
MBINU ZA KITAALAM ZA KUDHIBITI USALITI- 2
USALITI ni pasua kichwa. Unatesa na kuumiza wengi kwenye mapenzi. Walio ndani ya ndoa na ambao bado hawajaingia. Ni tatizo sugu ambalo kwa hakika linawasumbua wengi.
Ndiyo maana hapa kwenye All About Love tumelipa nafasi ya kulijadili kwa mapana ili tuweze kupambana nalo. Wiki iliyopita nilianza kwa kueleza namna ambavyo mtu anavyotakiwa kwanza yeye kuwa mwaminifu ili kumuweka mpenzi wake katika nafasi ya kumwamini na kuachana na mawazo ya kumsaliti.
Hebu twende tukaone vipengele vingine...
REJESHA NAKSHI ZA MAHABA
Mfano una mashaka mwenzi wako anakusaliti au unamhisi vibaya kutokana na namna alivyo makini zaidi na simu yake kipindi hiki. Lakini inawezekana kabisa, umeshafuma meseji zisizostahili kwenye simu ya mpenzi wako au umepata fununu kwamba anakusaliti.
Kubwa zaidi, inawezekana una ushahidi wa moja kwa moja kwamba anakusaliti. Anatoka na mtu mwingine. Usipaniki maana haitakusaidia, lazima usogee hatua moja mbele.
Huyo ni wako, tayari mpo kwenye ndoa, kuachana haiwezekani na hata kama inawezekana si suluhisho la mwisho, kwani yawezekana ukakutana na mwingine mwenye kasoro zaidi ya huyo.
Kitu cha kwanza kabisa kufanya ili kukomesha usaliti katika ndoa/penzi lenu ni kukumbusha yale ya zamani!
Unajua kuna umri fulani wanandoa wakifikisha, wanajisahau. Wanakuwa hawana jipya; si kwamba hawana jipya, bali hawataki kuonesha mambo mapya.
Nasema wanaweza kufanya mapya kwa sababu mwanandoa huyo huyo anayetoka nje kwa kukosa mapya kutoka kwa mpenzi wake, akienda nje, anakuwa mtundu balaa! Yapo, yanaonekana na watu wanayajua.
Mume ana nyumba ndogo na mke naye ana nyumba ndogo. Ngoma droo! Haina maana kabisa.
Hata kama mwenzi wako hajaanza katabia haka kachafu, lakini ni vizuri basi ukapambana ili kukomesha au kuzuia isitokee.
Wengi hujisahau baada ya kuingia kwenye ndoa, hili ni tatizo. Hebu twende tukaone zaidi.
(i) Kutoka pamoja
Hebu vuta picha, kipindi cha mwanzo wa mapenzi yenu, wewe umependeza na mwenzi wako naye pia, mnatoka pamoja na kwenda kuangalia bendi mnayoipenda, ufukweni au kwenye hoteli ya kifahari...mapenzi yanasonga jamani!
Huwezi kukaa na mkeo kila siku kwenye kochi lilelile, unamtazama kwa mtazamo uleule, halafu ukienda muziki unakutana na mademu wakali, unadata na kusema mkeo hana mvuto. Nani kasema?! Hebu mchukue, mpige pamba halafu nenda katika klabu za usiku, kama hamtagombana na wanaume wanaomkodolea macho!
(ii) Surprise
Si lazima iwe ya fedha kubwa, kitu chochote kinaweza kuwa surprise. Acha kujidanganya, hebu nunua hata maua ya elfu moja, pulizia manukato safi, halafu mpe ukimwambia; “Nakupenda baby.” Unataka surprise gani zaidi ya hiyo?
Kila anapokuwa anaona zawadi yako, atajihisi mgumu kumkubalia Pedeshee nanilii anayemsumbua kila anapokwenda buchani. Akili kichwani mwako mtu mzima!
(iii) Badili mazingira
Achana na ulimbukeni wa kila siku kukutana na mkeo sehemu moja, mbona zamani mlikuwa mnatoka na kulala nje ya mji au hotelini? Kuna mkono unapofikia, hata ukimchukua mwenzi wako na kwenda naye kwenye hoteli za kawaida bado utakuwa umebadilisha mazingira na utaonekana mpya.
Kumbuka kinachotafutwa hapa ni upya wa ndoa na mapenzi na kumfanya mwenzi wako asiwe na wazo la kusaka nyumba ndogo.
SAKA MSISIMKO ZAIDI
Ili penzi liendelee kuwa imara lazima utafute msisimko zaidi, yapo mengi ambayo yanaweza kuongeza msisimko katika penzi lako. Haiwezekani rafiki yangu uwe unarudi nyumbani saa tano usiku kila siku, unadhani utamwona mkeo ana tofauti?
Hapa ni kujidhibiti mwenyewe, maana usipokuwa makini, unaweza kushangaa unamdharau mkeo na kumuona hana mvuto kabisa. Huo mvuto utauona wapi kama kila ukija unamkuta amevaa kanga moja anataka kulala?
Utamuona wa kawaida na mwisho wa siku utaamua kutafuta kitulizo nje, ambapo mapenzi ndani yatapungua na si ajabu na yeye akaamua kusaka mahali pa kupumzisha moyo wake.
Mwanasaikolojia mmoja amewahi kuandika katika kitabu chake kuwa ili uzidi kumuona mpenzi wako mpya kila siku, lazima umfanye rafiki yako nambari wani.
Alisema: “Mke/mume lazima awe rafiki yako wa kwanza, unadhani utamuonaje wa muhimu kwako, kama hampati muda wa kuwa pamoja mkazungumza kirafiki?
“Tunashauri wanandoa wawe na muda wa mzaha, kutoka pamoja, kujadiliana mambo mbalimbali kirafiki ili kujenga ustawi bora zaidi wa ndoa yao.”
Akaendelea: “Huwezi kuwa na mkeo, kila siku yupo kwenye muonekano uleule, akakuvutia. Lazima leo awe amevaa sketi na blauzi, umshike mkono na kwenda naye beach, kesho mmekwenda pamoja Kariakoo kununua mahitaji. Utampenda daima.”
Alieleza kuwa mke kukaa ndani kihasarahasara ni kati ya mambo yanayoua mvuto na ushawishi wa kimapenzi ambao baadaye huzaa nyumba ndogo.
“Utakuta mwanamke akiwa chumbani na mumewe anakaa hovyohovyo, sehemu ya maungo yake yako wazi, sasa nini kitamvutia mumewe kama kila siku anamuona katika hali hiyo? Hapa lazima wanawake nao wawe macho jamani, vinginevyo hizi nyumba ndogo hazitaisha,” aliongeza.
Naamini kuna kitu umejifunza, wiki ijayo nitakuwa hapa katika mwendelezo wa mada hii, USIKOSE!
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment