ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 17, 2013

Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe.
Mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe, ameamua kukata mzizi wa fitna bungeni kwa kueleza wazi kuwa katika baraza lote la mawaziri lenye mawaziri 31 pamoja na naibu mawaziri 25 wanaofanya kazi ni 10 tu.

Mbali na kombora dhidi ya mawaziri, pia amewashambulia wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa wamesahau kazi iliyowapeleka na sasa wanafanya siasa bungeni.
Filikunjombe aliyasema hayo jana wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2013/14 bungeni mjini Dodoma.


Kuhusu Mawaziri, alisema wakati Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, anaapa bungeni alisema atailinda Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini sasa wanalindana wao na katiba wameiweka pembeni.

"Ukitazama kwa haraka haraka mawaziri wapo 60 mawaziri na manaibu wao ni (waliopo ni 57), wanaofanya kazi hawapiti 10 na ninaweza kuwataja kwa majina…liko jambo bayana na la wazi kuwa elimu yetu imeshuka ni kweli takwimu zinaonyesha kuwa sekondari, shule zimeongezeka kutoka 1,700 hadi 4,000," alisema.

Alisema ni kweli idadi ya wanafunzi wanaofaulu imeongezeka kutoka 400,000 hadi kufikia zaidi ya milioni 1.5 kwa mwaka 2006: “Lakini mimi niseme ni afadhali ya kuwa na wanafunzi 400,000 tu pekee kuliko kufaulisha wanafunzi milioni 1.5 hawajui kusoma na kuandika.”

“Tunafaulisha na kupeleka wanafunzi wanaokwenda kusoma kidato cha kwanza ambao hawajafaulu ni nafuu kuwa na wanafunzi wachache, wenye ubora kuliko kuwa wanafunzi wengi wasio na ubora,” alisema.

Alisema anawashangaa wabunge wenzake ambao wamekuwa wakipiga kelele kuwa matokeo ya kidato cha nne yamekuwa mabaya  na kwamba walipaswa kupigia kelele mwaka 2011 baada wanafunzi 11,000 waliofaulu kujiunga na sekondari huku wengine wakiwa hawajui kusoma, kuhesabu wala kuandika.

“Kama walioingia form one (kidato cha kwanza), wako vile watakaotoka watakuaje? Na takwimu kwamba elimu inashuka ni takwimu za serikali. Tume zilishaundwa, Tume ya Mzee Francis Liboyi iliundwa na kutumia fedha nyingi,”alisema na kuongeza kuwa:
“Badala ya watu kuwajibika tunaunda tume nyingine ili kufunika kombe ili mwanaharamu apite. Tunaweza kusema huo ni upepo utapita, lakini Watanzania wanajua, Watanzania wanaona.”

Alisema ingawa elimu ya msingi inasemwa kuwa ni bure, lakini si kweli na kwamba mara ya mwisho ada ilipofutwa ilikuwa ni Sh. 3,000 lakini leo hii katika jimbo lake la Ludewa, wanafunzi wanalipa Sh. 6,000 hadi Sh. 16,000.

Alishauri ni vyema kurudisha ada na kutangaza kuwa elimu ya msingi si bure, hali itakayowasaidia wazazi kujiandaa kulipa.

“Tunawaambia wazazi elimu ya msingi itakuwa ni bure huku tunatoza michango zaidi ya ada. Elimu yetu si nzuri na dhana ya uwajibikaji haipo, tunaishia kuunda tume,”alisema na kuongeza kuwa:

“Ukiona imeundwa tume ujue kuwa mambo yamekwisha. Tume nyingi zinaundwa na matokeo yake hatuyaoni. Tume nyingi zinaundwa na kuwekwa katika makabrasha, zikisema huo ni upepo utapita.”

Mbunge huyo ambaye amekuwa mwiba kwa chama chake bungeni mara nyingi, alisema badala ya wabunge wa CCM kuwajibika wanapoteza muda mwingi katika kuwajadili wabunge wa upinzani ambao ni wachache.

“Sisi ambao ni wazazi kimsingi tukiwajibika kwa wananchi hata wapinzani hawa hawatakuwa wapinzani watarudi. Kipimo chetu kiwe ni utendaji kazi na siyo kulumbana bila msingi. Tunakuja huku bungeni tunafanya kazi za Nape Nnauye (Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM)," alisema na kuongeza:

“Nape Nnauye atafanya kazi gani? Mheshimiwa Spika ndiyo maana unasema kuna matusi kwa sababu watu wameacha kufanya kazi zao wanafanya kazi za watu wengine.”
Alisema kuna mifano mizuri ambayo inaonyesha kuwa wakifanya kazi kwa mafanikio wapinzani wanaelewa na kujiunga na CCM. 
  
“Kuna mawaziri hapa walikuwa upinzani wameelewa kuwa tunafanya kazi vizuri wamerudi CCM… sisi tusiwabeze kila kitu upinzani, tubadilike. Sisi tukiwapenda na kuwaheshimu wataacha kutudharau na kututukana kila siku,” alisema.  
 
Aidha, alisema kuwa wananchi katika jimbo lake wanataka vitu vichache ikiwamo meli katika ziwa Nyasa kama walivyoahidiwa na Rais.

“Niseme kuwa kama hatupati meli mpya katika Ziwa Nyasa tutakwenda kuandamana, tutavaa sare zetu za CCM, suruali nyeusi na masharti yetu ya kijani, tutakwenda kuandamana barabarani bila kujali kuwa ni Jumatatu ama Jumapili,” alisema.

Alihoji wananchi wa Wilaya ya Ludewa wamekosa nini kwa kuwa wilaya zote zina barabara na kwamba ni lazima kuwapo kwa barabara ya lami kuanzia Njombe hadi Ludewa.

Alisema kuwa wamechoka na staili ya mfumo wa uongozi kwa kuwa kila wanapouliza kuhusiana na ujenzi wa chuo cha Ufundi Stadi (Veta), wamekuwa wakijibiwa kuwa wapo katika upembuzi yakinifu.

“Siungi mkono hoja kwa sababu kila anayeona, atakuwa shahidi kuwa Serikali yetu imekuwa siyo serikali sikivu kwa vitendo na serikali yetu imekuwa na tabia ya kufunika kombe ili mwanaharamu apite,” alisema na kuongeza kuwa:

“Siungi mkono hoja kwa sababu Serikali yetu imevaa miwani ya mbao na haisikii.”
Hata hivyo, alikatishwa na Spika wa Bunge, Anne Makinda, ambaye alimtaka aondoe maneno hayo na akakubali kuyaondoa. “Inasitikisha sana viongozi wa Serikali yetu wamekuwa wakifanya mambo wanayoyataka wao viongozi hawafanyi mambo wanayotaka wananchi,” alisema.

Filikunjombe aliwataka viongozi na wabunge wenzake hasa wa chama tawala kubadilika na kuacha kubeza kila hoja za upinzani.

“Tusiwabeze badala yake tuchukue hoja zao na kuzipima ili tuzifanyie kazi.  Kuna msemo usemao ukiona kobe yuko juu ya mti ujue amebebwa na kuwekwa pale. Sisi tumepewa dhamana ya kuongoza Watanzania na kuwatumikia...tusiichezee,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Poa sana FIKILI kunjombe ,Ni Mbunge pekee Unaefikiri kwa kina .