ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 6, 2013

MMILIKI WA JENGO LILILOLETA MAAFA DAR APEWA SIKU 30 KUBOMOA JENGO LAKE LINGINE LA GHOROFA 16

 Mwenyekiti wa kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli. akiongea leo wakati kamati hiyo ilipotembelea eneo lilikoporomoka ghorofa mtaa wa Indira Ghandi jijini Dar es salaam leo, akiwa ameongozana na wajumbe wa kamati hiyo pamoja na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Profesa AnnaTibaijuka. 

Kamati hiyo imeziamuru halmashauri za Wilaya ya Temeke, Ilala na Kinondoni kufanya tathmini ya majengo yote na kuchukua hatua mara moja zitapogundulika zimejengwa chini ya kiwango.

Tayari watu 11 wanaotuhumiwa kuhusika katika ujenzi wa ghorofa lililoporomoka wamefikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya kuua bila kukusudia 
 
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Profesa AnnaTibaijuka akiwa eneo la jengo lilioporomoka. Nyuma yake ni jengo ambalo linajengwa na mjenzi yule yule aliyejenga liliporomoka. Kamati hiyo imetoa siku nne kwa mjenzi kubomoa jengo hilo ambalo linasemekana nalo limejengwa chini ya kiwango. 
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Profesa AnnaTibaijuka na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira Dk TerezyaHuvisa wakimsikiliza   Mwenyekiti wa kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli.
 Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,Profesa AnnaTibaijuka  na  Mwenyekiti wa kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli.
  Mwenyekiti wa kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, James Lembeli akijadili jambo na Bw. Azim Dewji pamoja na mjumbe wa kamati Mhe Zakhia Meghji. Picha na mdau Sujit Bhojak


Dar es Salaam. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, ametoa siku 30 kwa mmiliki wa jengo la ghorofa 16, lililopo Mtaa wa Indira Gandhi katikati ya jiji, Ally Raza kulibomoa jengo hilo baada ya kubainika alilijenga chini ya kiwango.
Kadhalika Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira imeiagiza Halmashauri ya Manispaa ya Ilala, kufanya uchunguzi wa ubora wa majengo mengine matano yanayomilikiwa na Raza ambaye pia ni mmiliki wa jengo lingine la ghoroga 16 lililoporomoka wiki iliyopita jijini Dar es Salaam kama yako katika viwango vinavyokidhi.
Jengo hilo lililoporomoka lilisababisha vifo vya watu 36, majeruhi 17 na uharibifu wa mali ikiwamo magari linamilikiwa na Raza.
Jengo hilo lilikuwa likijengwa na Kampuni ya Lucky Construction Limited ambayo ni mali ya Diwani wa Kata ya Goba (CCM) Wilaya ya Kinondoni, Ibrahim Kisoki ambaye pia alijenga jengo jingine jirani na la awali, imetolewa amri ya kufanyika kwa utafiti kubaini kama limekidhi viwango.
Profesa Tibaijuka akizungumza mbele ya Kamati hiyo walipofanya ziara katika jengo hilo jana, alisema uchunguzi wa awali wa kuporomoka kwa jengo hilo umebaini kuwa jengo lililoko mkabala, pia lilijengwa chini ya viwango.
“Ninaagiza jengo hilo kuwa libomolewe ndani ya siku 30 kwa gharama za mmiliki na akikaidi atalipishwa faini ya asilimia mbili ya gharama ya kuendeleza pasipokuwa na kibali kwa kila siku hadi atakapotekeleza agizo hilo,” alisema Profesa Tibaijuka na kuongeza;
“Makazi haya yanatakiwa kujengwa majengo yasiyozidi ghorofa 10, lakini katika hili ghorofa ambalo linatakiwa kubomolewa kwanza kiutaalamu halikuzingatia vigezo kutokana na kujengwa kwenye kiwanja chenye mita 150 ambacho ni kidogo.”
Naye Mwenyekiti wa Kamati hiyo, James Lembeli alisema kuna taarifa kwamba mmiliki wa jengo anamiliki majengo mengine ambayo hivi sasa yanakaliwa na watu pia yamezua hofu, hivyo yanatakiwa kufanyiwa uchunguzi.
“Kutokana na majengo yake mawili ambayo tayari yameleta utata kwa kuonekana kujengwa chini ya viwango, hivyo tunataka majengo mengine anayomiliki, Manispaa ya Ilala iyafanyie uchunguzi mapema ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea,” alisema Lembeli.
Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Dk Terezya Huvisa amewataka watu wanaotaka kujenga majengo yenye zaidi ya ghorofa sita kufika ofisini kwake kupata vibali vya ujenzi.
“Mtu yeyote anayetaka kujenga jengo zaidi ya ghorofa sita anatakiwa kuomba kibali wizarani na wao kupitia Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) watatoa kibali cha kujengwa au kutojengwa kutokana na uchunguzi wa sehemu husika,” alisema Dk Huvisa.
Habari na Mwananchi

2 comments:

Anonymous said...

Reactive nation with reactive culture. People are reacting after the fact. How many buildings are you going to demolish? What at disaster.

Anonymous said...

zakhia meghji siku hizi ana jifunika mashallah