ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, April 13, 2013

Kufanya hivi si kujua mapenzi bali ulimbukeni

NATUMAI wote ni wazima wa afya. Kabla ya yote ningependa kuwafahamisha wote wanaouliza maswali kwa ujumbe mfupi (sms), wapige simu moja kwa moja, kila atakayepiga simu ndiye atakayepata msaada wa haraka.
Baada ya ujumbe huo tuendelee na mada yetu. Leo napenda kuchukua fursa hii kuwaelewesha wale malimbukeni wa mapenzi wanaojitoa akili na kujifanya mapenzi wanayajua sana kuliko watu wote.
Nina maana gani kusema hivi?
Kumekuwa na matukio ya kukinaisha hasa sehemu za mjumuiko wa watu ambapo utakutana na watu ambao hufanya mambo ya faragha mbele za watu bila aibu.
Unamuona mtu na mpenzi wake mbele za watu bila kuangalia wapo eneo gani wananyonyana ulimi huku wakigugumia kimahaba. Wengine kushikana sehemu za siri bila aibu eti kisa kwa sababu wanapendana.

Juzi, nikiwa ndani ya daladala tulikuwa tumejaa kama ilivyo kawaida. Mmoja wa abiria alipokea simu ambayo ilionyesha inatoka kwa mpenzi wake, kwa vile hakuwa mstaarabu wa kujua nini maana ya mapenzi na maneno yake hutumika upande gani, ndiyo maana tulijua anayezungumza naye ni nani.
Jamaa alianza kuzungumza kwa sauti ya juu kuonyesha anajua mapenzi kwa kuzungumza maneno mengine ambayo kwa mtu mwenye akili timamu angeona aibu kuyatamka kwenye kadamnasi.
Yaani alikuwa akizungumza yeye tu huku akimpiga mabusu huyo mpenzi wake bila kuangalia mle ndani ya daladala kuna abiria wa aina gani.
Jamaa alishuka njiani na kuwaacha watu wakimjadili kutokana na ulimbukeni wake. Tukio lile lilinifanya nishike kalamu kuyaeleza haya machache.
Ukweli usiopingika kwamba kuna baadhi ya watu, mapenzi wameyaanzia ukubwani au malimbukeni katika mapenzi.
Watu wa aina hiyo hujiona wao ndiyo wanaojua mapenzi kuliko wote. Watu hao wapo radhi kufanya chochote cha faragha mbele ya watu ili kuonyesha wanapenda. Ndiyo haohao huzungumza kwa sauti ya juu kwenye daladala kwa simu huku wakichombezana kwa maneno ambayo yana sehemu zake.
Lazima tuuthamini upendeleo tuliopewa na Mungu wa kukuumba mwanadamu mwenye akili timamu mwenye tofauti na mnyama. Hivi wewe mwanadamu unayeonyesha vitu vya faragha mbele za watu una tofauti gani na mnyama?
Tuelewe kuwa kuna vitendo na maneno ya kimahaba ambayo tunatakiwa kufanya na mpenzi wetu faragha na si mbele ya watu, pia lazima tujue matumizi ya simu, unatakiwa uzungumze nini na sehemu gani.
Kama mpenzio amekupigia simu ndani ya daladala au sehemu ya watu, mueleze ili akupigie baadaye tena sehemu muafaka.
Mnapokuwa katika hali ya kimahaba basi muangalie mazingira kama yanaruhusu, ni jambo la ajabu mpo kituoni au ndani ya daladala mnafanya mambo ya faragha mbele za watu bila aibu.
Siku zote mtu anayefanya mambo ya chumbani hadharani hata awe amevaa nguo akili zake huwa sawa na punguani. Mwanadamu uso wake umeumbwa kwa aibu, hufikiria kabla ya kutenda. Ukiwachunguza watu wenye vitendo hivyo utagundua ni wageni katika medani ya mapenzi au wana upungufu wa uelewa.
Kukumbatiana kushikana mikono ni jambo la kawaida, lakini kunyonyana ulimi au kushikana sehemu za siri mbele za watu ni matatizo ya kiakili, sehemu hizo zina mahali pake ambapo ni faragha.
Tuwe wastaarabu kwa kujiheshimu hasa mbele ya watu ili tuheshimke. Siku zote jiheshimu utaheshimiwa.

Kwa hayo machache tukutane wiki ijayo.

Global Publishers

1 comment:

Anonymous said...

WIVU TU WEWE SI AJABU HUKUWAHI HATA KUSHIKWA WALA KUPIGIWA SIMU KWANI KUBUSU NDANI YA DALADALA KUNA KUWASHA NINI? UMECHANGANYIKIWA NA WEWE PIA KUMJADILI MTU USIYE MJUA WAKATI HATA HAYUPO KWENYE BASI. KAMA MPENZI WAKE NDIYE ANAPENDA JE AFANYEJE? MIND YOUR OWN BUSINESS HUNA MTU KAZI KUSIKILIZA MAONGEZI YA WATU WENGINE DAAA WACHAWI UTAWAJUA TU.