Dar.Hatima ya uchaguzi mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania, itajulikana leo wakati Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza itakapotoa hukumu ya pingamizi dhidi ya kesi iliyofunguliwa na kuzuia uchaguzi huo na mgombea Richard Rukambura.
Wakati kesi hiyo ikiunguruma mahakamani Mwanza leo, ujumbe wa Shirikisho la Soka la Dunia (FIFA), ukiongozwa na Primo Cavaro, utakutana na Waziri wa Michezo, Dk Fenella Mukangara kujadili kuhusu uchaguzi huo.
Rukambura alifungua kesi namba 1 ya mwaka 2013 katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanzo akiomba mahakama kuzuia kufanyika kwa uchaguzi huo wa TFF ambao awali ulipangwa ufanyike Februari 24 na kesi hiyo ilianza kunguruma Februari 19 mwaka huu.
Katika madai yake, Rukambura alitaka Mahakama izuie uchaguzi huo na kumrejesha kwenye kinyang’anyiro cha urais kwa vile anaamini alienguliwa kwa hila.
Kamati ya uchaguzi chini ya Deogratius Lyato ilimwengua Rukambura kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi kwa kile kilichodaiwa kuwa ni kukiuka kanuni za uchaguzi kwa kujaza fomu mbili za kugombea kinyume na taratibu za uchaguzi wa shirikisho hilo.
Hata hivyo, baada ya kufunguliwa kwa kesi hiyo, TFF kupitia kwa wakili wake, Alex Mgongolwa waliweka pingamizi la kutaka kesi hiyo itupiliwe mbali kwa kuwa kwa mujibu wa katiba ya TFF masuala ya soka hayaruhusiwi kupelekwa kwenye mahakama za kawaida za kisheria.
Kufuatia hali hiyo, Jaji Amir Mruma leo atatoa hukumu ya mapingamizi hayo yaliyowekwa na TFF ama kuyatupa au la.
Hata hivyo tayari Rais wa TFF, Leodegar Tenga ameshaweka wazi msimamo wake kuwa Rukambura kwa kufungua kwake kesi mahakamani amejipalia mkaa wa moto na asahau kupata nafasi yoyote ya uongozi kwenye masuala ya soka kwa kuwa amekiuka katiba ya TFF, CAF na Fifa ambayo inazuia masuala ya soka kupelekwa mahakama za kawaida za kisheria.
Mbali na suala hilo la mahakamani, ujumbe wa Fifa ambao ulitarajiwa kuwasili nchini jana saa mbili usiku, utakutana na Waziri Dk Mukangara leo asubuhi na baadaye kukutana na wagombea sita walioenguliwa kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi huo na kamati ya uchaguzi chini ya Idd Mtiginjola na kisha kuomba marejeo ya rufaa zao.
Wagombea ambao hatima yao ipo mikononi mwa Fifa ni Jamal Malinzi, Michael Wambura, Hamad Yahaya, Eliud Mvela, Farid Nahd na Mbasha Matutu
Mwananchi
No comments:
Post a Comment