U-HALI gani mpenzi wa kona yetu, baada ya kuzungumzia madhara ya kuruka na kurukwa ukuta wiki mbili zilizopita, mada iliyowagusa wengi na kuona jinsi ndani ya uhusiano wetu mchezo huo umezoeleka.
Nina imani mmeona madhara ya kuucheza mchezo huo japokuwa wapo wasioamini, ila ipo siku watakubali nilichokisema lakini wakati huo wameishaumia.
Leo tutizame uhalisia wa mapenzi. Tumeona jinsi mapenzi yanavyowaumiza watu wengine na kukimbilia kujiua au kukonda kama wagonjwa.
Ukiuliza unaambiwa eti sababu ya mapenzi, lakini mbona nikiliuliza ‘penzi’ lenyewe linakataa kuua au kumtesa mtu!
Aliyempoteza ndugu yake kwa ajili ya mapenzi au anayeendelea kuteseka anamuona mapenzi ni muongo kwani yasingemkuta yale bila yeye.
Lakini nataka kupata ukweli kwa nini ‘mapenzi’ anasema yeye hahusiki kwa jambo lolote? Naye ananiuliza swali, namfahamu vipi yeye?
Jibu lake lilikuwa mapenzi ni furaha, faraja ya moyo, upendo wa dhati, huruma, kujali na kujitoa kwa ajili ya mwenzako.
Baada ya jibu langu ‘mapenzi’ ananiuliza swali “Katika majibu yako umeona sehemu gani nimeiona mimi ni mateso au mimi ni kifo kwa watu?”
Jibu kwa kweli linanitoa jasho na kunifanya nimuulize tena: “Sasa mapenzi kwa nini watu wanateseka kwa ajili yako na wengine kufikia kujiua?”
‘Mapenzi’ anajielezea: “Naomba leo nijiweke wazi, siku zote kwenye mapenzi ya kweli hateseki mtu wala kufa bali kwa maamuzi ya Mungu. Siku zote makosa yanatokea kwa uliyemkabidhi moyo bila kujua ni mtu sahihi kwao na kama ana upendo wa kweli kwako.
“Mtu uliyempa penzi lako ni kweli anakupenda au anakutamani kwa ajili ya kitu? Makosa mengi hutokea wakati wa kuchagua au kumkubali mtu. Ukikosea lazima mapenzi yataonekana mabaya na watu kufikia hatua ya kusema hawatapenda tena maishani mwao.”
Sasa niendelee kukupa darasa, mbegu ya mapenzi ukiipanda kwenye moyo wenye rutuba ya upendo huwezi kuyaona mabaya. Wengi tumekuwa tukikurupuka katika na kuamini hisia zetu zipo sahihi kwa kile tunachokitaka bila kuangalia upande wa pili kwamba ninayempenda naye ananipenda.
Kama hana mapenzi na wewe lazima utayachukia, lakini siku zote mapenzi ya kweli yapo kama mafuta yasiyochanganyika na maji.
Kuna sehemu tunakosea kama alivyosema ‘mapenzi’ kuwa kabla ya kumkabidhi mtu moyo wako, anatakiwa mtu huyo awe ni sahihi na kweli amevaa vazi lenye huruma, upendo, kujali na kuthamini. Hakika utalifurahia penzi na kuiona ile pepo ya duniani.
Lakini ukimkabidhi moyo wako asiye sahihi lazima utayachukia. Jiepushe kurudia kosa moja zaidi ya mara mbili, usiwe mwepesi kuugawa moyo wako ovyo. Siku zote maumivu ya moyo unayabeba mwenyewe, hivyo unatakiwa kuwa makini unapoingia katika uhusiano mpya.
Kila kiumbe kinahitaji kupendwa, vilevile anayependwa naye anatakiwa kurudisha upendo kwa vile wapenzi huwa pacha kwa kila mmoja kumpenda mwenzake na kumlinda.
Kwa maneno hayo inaonyesha wazi kabisa kinachoumiza si mapenzi bali ukatili wa watu wasio na huruma na upendo wa mwenzao na kuutumia kama fimbo ya kumpigia.
Siku zote amini mapenzi ni furaha wala si mateso, bali wanaotesa siku zote huwa wenye tamaa kuliko kupenda.
Kwa hayo machache tumeona mapenzi hayaui wala hayatesi bali uliyempa penzi lako si sahihi.
Tukutane wiki ijayo.
GPL
No comments:
Post a Comment