ANGALIA LIVE NEWS

Monday, April 1, 2013

MAKUNDI YA WANAUME NA MITAZAMO YAO YA KIMAPENZI KWA WANAWAKE -10

MFANO huo wa Rehema ambao niliutoa wiki iliyopita, wakati nikieleza bahati mbaya ambayo wanaume wa kundi la tatu (watu wa gubu) wanaweza kuwa nayo, unatosha kukufanya utambue umuhimu wa utulivu kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Hii ndiyo sababu ya kueleza kuwa moja ya bahati mbaya ambayo wanaume wa kundi hili wanayo ni kusalitiwa na wenzi wao wa maisha. Yaani jazba, ukali wako na kadhalika, vinasababisha mwenzi wako atafute tulizo nje. Ukigundua ni maumivu, hata usipojua, ni hatari kwa afya yako. Maradhi mengi.
Tatizo lingine ni kuogopwa. Kwa vile wana gubu, hata uchangamfu wao hupatikana kwa mgawo. Wake zao hunywea kila wanapogundua kwamba kisirani kimeanza. Watoto na memba wengine wa familia, hupatwa mchecheto ndani ya nyumba.
Hiyo siyo sifa nzuri kwa mwanaume. Baadhi huona sifa kwamba wanaogopwa lakini shika ukweli huu kwa faida yako kwamba wengi wamekosa mengi mazuri kutokana na hulka zao za jazba na hasira za haraka. Wivu unaozaa gubu ni kichocheo cha nyumba nyingi kuparanganyika.
Mwanaume ni vizuri akawa na subira, kuna mambo ya kumezea, mengine ya kutafakari kabla ya kuchukia. Bahati mbaya kwa wale wanaounda kundi hili ni kwamba wao huwa hawangoji tafakari, badala yake huwa na hasira za utadhani swila anavyojaza sumu mdomoni kila anapohisi kuna adui.
Tabia hiyo ya gubu, huwafanya wawe wanachemka mara kwa mara. Huchukua uamuzi wa haraka ambao baada ya muda hugundua kwamba unawagharimu wao wenyewe. Baadaye wakishagundua waliamua bila kutafakari, hupata shida kuomba radhi na kuwarejesha wenzi wao kwenye hali ya kawaida.
Tatizo lingine kubwa ni kwamba hawana huba (nonromantic). Ni wakorofi na wapandisha jazba. Huba hupatikana kwa mtu aliyetulia, akili ipo sawa. Hivyo basi, pamoja na mengine yote ambayo yameshatajwa, hili pia ni janga ambalo huwaondolea wanaume wa kundi hili, alama za ushindi kwenye mapenzi.

KUNDI LA NNE
Linahusisha wanaume ambao ni vema kuwaita makini. Hawa ndiyo walio tayari kuishi katika ndoa. Wasioangalia mambo madogomadogo kwenye mapenzi, bali huzingatia masuala ya msingi, yenye sura ya kujenga mapenzi, ndoa, nyumba na familia bora.
Hii ni aina ya wanaume ambao, daima huamini katika kufundisha. Kwamba mwanamke anaweza kuwa na hulka mbaya au historia chafu lakini akitua kwa mwanaume anayeunda kundi hili, hubadilika kwa urahisi, kutoka ubaya wa shetani hadi uzuri wa malaika.
Kama hujawahi kushuhudia basi mifano ipo. Mwanamke anakuwa na kila aina ya sifa mbaya. Mlevi, mhuni, anabadili wanaume kama nguo. Mtaani anasifika kwamba ameshindikana. Baadaye anakuja kutulia kwa mumewe mpaka watu wanashangaa.
Tena wanaoshangaa zaidi ni wale waliokuwa wanapaza sauti wakisema kuwa ndoa haitadumu. Wakamponda mwanaume kwamba amejiingiza kichwakichwa kwa mwanamke ambaye hajui historia yake. Ni kawaida ya binadamu kusemasema.
Kwa mkazo, naomba uzingatie kuwa si kila mfanya uchafu ni mchafu, siyo wote wanaokunywa pombe ni walevi. Historia ya maisha ya mtu, inaweza kumfanya malaika afanane na shetani. Itakuwa ni ngumu kwako kutambua umalaika wake, ikiwa utakimbilia kumhukumu kwa muonekano wake.
Siku zote, vitu vizuri hutafutwa.
Itaendelea wiki ijayo.

Global Publishers

No comments: