ANGALIA LIVE NEWS

Friday, April 19, 2013

Mbowe amhoji Spika kufukuzwa wabunge

Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (pichani), ameomba mwongozo kwa Spika wa Bunge, Anne Makinda, ikitaka kufahamu lini wabunge sita waliopewa adhabu ya kutohudhuria vikao vitano vya Bunge wataruhusiwa kwa kuwa kanuni iliyotumika kuwaadhibu haikuwa sahihi
Mbowe aliomba muongozo kwa mujibu wa kifungu cha 68 (7) cha Kanuni za Bunge.

Alisema kifungu hicho kinasema “Hali kadhalika Mbunge anaweza kusimama wakati wowote ambapo hakuna Mbunge mwingine anayesema na kuomba ‘mwongozo wa Spika’ atoe ufafanuzi kama jambo hilo linaruhusiwa au haliruhusiwi kwa mujibu wa kanuni na taratibu za Bunge na majibu ya Spika yatatolewa papo hapo au baadaye kadri atakavyoona inafaa.” Alisema: "Kwa mujibu wa kanuni ambazo zinasimamia Bunge letu jana (juzi), Naibu Spika (Job Ndugai), katika kipindi chake cha jioni wabunge sita walitolewa nje…walipewa pia adhabu ya kutohudhuria vikao vya Bunge vitano adhabu iliyotolewa papo kwa papo.”

Alisema kanuni inayompa mamlaka ya kumtoa Mbunge kwa muda wa siku tano ni ya 73 (3) ambayo inasema kuwa Mbunge anaweza kufukuzwa kama hatatoa uthibitisho wa kutosha.
Kifungu hicho kinasema “Endapo Mbunge yeyote atatakiwa kuthibitisha ukweli wa maneno aliyoyasema na hadi kufikia mwisho wa muda aliopewa, amekataa ama ameshindwa kutoa uthibitisho huo, Spika anaweza kumsimamisha mbunge huyo asihudhurie vikao vya Bunge visivyozidi vitano.”

Alisema katika mjadala huakulitokea hali ya kutokuelewana kati ya Ndugai na wabunge hao na katika mambo ya msingi walitegemea kifungu namba 74 (1) ambacho kinataka mbunge kama huyo kupelekwa katika Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge. Kifungu hicho kinasema, “Spika anaweza kutaja jina la Mbunge kwamba amedharau mamlaka ya Spika na kisha kupeleka jina hilo kwenye Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.

“Mheshimiwa Spika naomba mwongozo wako wabunge wale walitolewa bungeni ni lini watarudi?” alihoji.

Hata hivyo, Spika alisema kuwa kanuni hizo hizo zitatoa mwongozo muda huo huo ama katika muda anaoona unafaa na kwamba atautolea baadaye. Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai (Chadema), aliomba mwongozo huo jana muda mfupi baada ya kipindi cha maswali na majibu bungeni.

Wabunge walioadhibiwa na Naibu Spika, Job Ndugai, na majimbo yao katika mabano ni Tundu Lissu (Singida Magharibi), Joseph Mbilinyi (Mbeya Mjini), Peter Msigwa (Iringa Mjini), Highness Kiwia (Ilemela), Godbless Lema (Arusha Mjini) na Ezikiel Wenje (Nyamagana).

Adhabu hiyo ilikuja mara baada ya Lissu kutakiwa kukaa chini wakati akitaka kuomba mwongozo wakati Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM), Mwigulu Nchemba aliyekuwa akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais (Utawala Bora).

Wakati huo huo, Chadema, mikoa ya Rukwa na Katavi, kimeanza maandalizi ya maandamano yenye lengo la kupinga kile walichokiita upendeleo unaoonyeshwa na Spika pamoja na Naibu wake.

Wakizungumza na gazeti hili jana, Mwenyekiti wa chama hicho wa mikoa hiyo, John Mallac na Katibu wake Ozemu Chapiter, walisema lengo jingine la maandamano hayo ni kupinga maneno yaliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Stella Manyanya wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais.

“Tumeanza kuwasiliana na wanachama na wananchi wengine wa mikoa ya Rukwa na Katavi kuhusiana na maandamano tunayotaka kufanya kupinga vitendo hivyo,” alisema Chapiter.

Alisema maneno yaliyotolewa na Manyanya ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa kwamba aliwataka polisi kumkamata endapo atatukana katika mkutano wa hadhara ina lengo la kumkashifu.

“Ndiyo maana siku zote sisi tumekuwa tukisema kiti cha uspika hakihitaji kuwa na mtu ambaye ni mwanachama wa chama chochote cha siasa ili kuweka usawa wakati wa kuchangia,” alisema Mallac.o
CHANZO: NIPASHE

No comments: