
Kiungo wa Yanga, Frank Domayo (kushoto) akimnyoosha misuli mshambuliaji Said Bahanuzi, katika mazoezi kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga. Yanga leo itacheza dhidi ya Mgambo Shooting. Picha na Salim Mohammed.
Dar es Salaam. Vinara wa Ligi Kuu, Yanga watashuka kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga kuikabili JKT Mgambo kwa lengo moja tu la kupata pointi tatu muhimu katika mbio zake za kusaka ubingwa.
Hatua kubwa ya kwanza waliyoifanya Yanga kuelekea kurejesha taji Jangwani ni kumpoteza kwenye mbio za ubingwa hasimu wake mkubwa, Simba ambaye sasa anashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.
Jumamosi iliyopita, mabingwa hao ‘watarajiwa’ msimu huu waliwashushia kipigo kinene maafande wa JKT Oljoro kwa kuinyoa mabao 3-0 na kufikisha pointi 52, ambazo Simba hata wakifurukuta vipi hawawezi kuzifikia.
Hofu kubwa kwa Yanga inaweza kuwa kwa wapinzani wao kwenye mbizo hizo, Azam FC inayoshika nafasi ya pili kwa kuwa na pointi 47, pia wakiwa mbele kwa mchezo mmoja.
Yanga ikifanikiwa kuibuka kidedea leo itafikisha pointi 55, ambazo zinaweza kufikiwa na Azam pekee, lakini kwa kuomba Wanajangwani hao wapoteze mechi zao zilizobaki.
Wekundu wa Msimbazi, Simba wako nafasi ya nne baada ya kukusanya pointi 36, ambapo siyo tu wamepotea kwenye mbio za ubingwa msimu huu, bali hata nafasi ya pili kwao ni majaliwa kwa vile mbali ya kuwamo katika uwezekano wa kutwaliwa na Azam pia inatolewa udenda na Kagera Sugar iliyoko nafasi ya tatu ikiwa na pointi 37. Mgambo walio katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wakiwa na pointi 24, watashuka dimbani kwa lengo la kulipa kiasi baada ya kuhujumiwa mabao 2-0 katika pambano la kwanza lililoamriwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Wapiganaji hao pia wataingia uwanjani kwa lengo la kusaka ushindi ili kujiweka mbali na janga la kushuka daraja msimu huu.
Kocha wa Yanga, Ernest Brandts mara baada ya mchezo dhidi ya Oljoro alisema kikosi chake kiko imara kwa sasa baada ya kukipa mafunzo ya zaidi ya wiki moja ya namna ya kufunga.
Mafunzo hayo yalizaa matunda kwenye mchezo dhidi ya Oljoro, kwani baada ya kufululiza na ushindi kiduchu wa bao moja kwa mechi kadhaa, waliibuka na ushindi mzuri kwenye mechi dhidi ya Oljoro.
Mafunzo hayo yalizaa matunda kwenye mchezo dhidi ya Oljoro, kwani baada ya kufululiza na ushindi kiduchu wa bao moja kwa mechi kadhaa, waliibuka na ushindi mzuri kwenye mechi dhidi ya Oljoro.
Ligi hiyo iliyofikia hatua ya lala salama pia itashuhudia Kagera Sugar ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba kukwaana na wanyonge Toto Africans wanaokamata nafasi ya 11 wakiwa na pointi 22.
Uwanja wa Manungu ulioko Turiani mkoani Morogoro, wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 4,000 utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya Mtibwa Sugar yenye pointi 33 na Oljoro JKT yenye pointi 28.
Wakati huohuo; Jana Coastal Union ililazimishwa suruhu na JKT Ruvu kwenye Mkwakwani.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment