ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, April 4, 2013

Ndolanga kuichongea TFF Fifa

Dar es Salaam. Wakati ujumbe wa Shirikisho la Soka Dunia (Fifa) ukitarajiwa kuja nchini Aprili 16, kufanya tathmini ya mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Mwenyekiti wa zamani wa Chama cha Soka Tanzania (FAT), Muhidin Ndolanga amesema atalichongea shirikisho hilo mbele ya ujumbe wa Fifa akilituhumu kwa utendaji mbovu.

Bila kutaja utendaji huo mbovu, Ndolanga alisema siyo yeye pekee atakayeukosoa utendaji mbovu wa TFF, bali pia wadau wengine ambao hakuwataja majina, wataichongea TFF mbele ya Fifa.

Akiongea na Mwananchi jana, Ndolanga alisema Fifa hawana wanachokijua kuhusu TFF, na kwamba watashangazwa na taarifa za mchakato wa uchaguzi ulivyoendeshwa.
“TFF watasema yao na sisi wadau tutasema yetu. Naamini Fifa watashangazwa sana,” alisema Ndolanga ambaye ni mjumbe wa heshima wa shirikisho hilo.

“Haiwezekani TFF ifanye madudu na bado watu wakae kimya. Hii siyo mali ya mtu binafsi, tutaongea yote.” Aliongeza: “TFF haipaswi kuingiliwa katika utendaji wake, pia Fifa haiwezi kuvumilia utendaji mbovu wa TFF.”

Hii siyo mara ya kwanza kwa Ndolanga kuukosoa utendaji wa TFF chini ya Rais Leodegar Tenga, kwani amekuwa akifanya hivyo mara kwa mara kwa madai ya kutokuridhishwa kwa kile alichokitafsiri utendaji mbovu.

Kwa upande wake mgombea wa nafasi ya urais aliyeenguliwa, Jamal Malinzi aliliambia Mwananchi jana kuwa, amejipanga kueleza malalamiko yake mbele ya ujumbe wa Fifa.
“Nina mambo ya kuongea, lakini siwezi kufanya hivyo kwa sasa mpaka muda utakapofika,” alisema Malinzi kwa ufupi alipoombwa kueleza alivyojipanga pale atakapokutana na ujumbe wa Fifa. Uchaguzi wa TFF ulisimamishwa kutokana na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wagombea kupinga kuenguliwa kushiriki ambapo baadhi wamefungua kesi.
Mwananchi

No comments: