Ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa 16 jijini Dar es Salaam na kuua watu 36 imeendelea mjadala na safari hii kada wa CCM na Mjumbe wa Baraza la Wawakilishi, Mohamed Raza, amejitosa na kusema kuwa ni ya kujitakia.
Raza ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Uzini Zanzibar na mfanyabiashara maarufu, alisema hayo alipozungumza na magazeti ya kampuni ya The Guardian jijini Dar jana.
“Ajali za kuanguka mara kwa mara kwa majengo ya maghorofa ni kama ya kujitakia, kwa sababu serikali mpaka sasa imeshindwa kuifanyia kazi ripoti ya kamati ya uchunguzi iliyoundwa na aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ya kuchunguza hali ya majengo jijini Dar,” alisema Raza.
Raza alisema iwapo serikali ingeyachukua mapendekezo yaliyopo katika ripoti ya Lowassa, basi kusingekuwepo na hali hatarishi ya kuhofia usalama wa majengo hayo jijini Dar es Salaam.
Alisema hafurahishwi na ajali hizo za mara kwa mara za kuanguka kwa majengo na kusababisha vifo vya Watanzania, lakini zinaonekana ni za kujitakia kutokana na kutokuwa na ufuatiliaji wowote kutoka serikalini.
“Kwa jengo hilo linasemekana lilitakiwa kujengwa ghorofa 10, lakini kwa tamaa ya mmiliki wake akaongeza na kufikia 16, sasa wahusika ambao ni serikali wameacha majengo mangapi ya namna hiyo jijini,” alihoji Raza.
Aidha, Raza alisema pamoja na wahusika waliosababisha uzembe hadi kuanguka kwa jengo hilo, bado ana wasiwasi wa sheria kuwabeba na kisha serikali kutwishwa mzigo wa kulipa fidia.
Raza alisema baada ya kuzuia kusitokee majanga kama hayo, lakini serikali imekuwa ikitumia gharama kubwa ambazo si za lazima katika kukabiliana na matukio mbalimbali ambayo yangeweza kuepukika.
“Hapa hatuwezi kusema tumepoteza watu 36 tu, bali wale waliokufa baadhi yao walikuwa wakitegemewa na familia zao, lakini kwa uzembe wa watu wachache wameacha yatima wengi bila kutegemea,” alisema.
Pia alisema kutokana na tukio hilo lililotokea lazima sheria iweze kuchukua mkondo wake na kutowaonea aibu wahusika hata kama ni makada wa chama kinachotawala.
Raza alisema kutokana na Jiji la Dar kuwa kitovu cha biashara na maofisi, lazima ukaguzi wa mara kwa mara wa majengo ufanyike.
Alishauri pale yanapotokea majanga ya kizembe kama hayo, wahusika wasikimbizwe mahakamani haraka, bali mashitaka yaandaliwe kwa umakini na wanasheria wa serikali, wakaguzi wa majengo na wataalamu wengine ili serikali isiumbuke.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment