ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 10, 2013

SMZ yakiri kuathiriwa mabadiliko tabianchi

Zanzibar. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imekiri kuathirika na tabianchi ambayo kwa kiwango fulani visiwa hivyo vibakabiliwa na tishio la mmomonyomko wa radhi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Fatma Abdulhabib Fereji alisema hayo wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Mtambwe (CUF), Salim Abdallah Hamad aliyetaka kujua athari ya mazingira ambayo imeonekana maeneo ya visiwa vya Zanzibar.
Pia, Salim alitaka kujua jinsi wizara ilivyojipanga kupambana na uharibifu huo, ili wananchi waweze kutumia ardhi yao ipasavyo.
Waziri Fereji alisema ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ikiwamo kuingia maji ya chumvi kwenye mashamba ya wakulima, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, imekuwa ikiwahamasisha na kuwaelimisha wadau maeneo yalioathiriwa kupanda miti kwa wingi.
Alisema wakati mwingine ikibidi kujenga matuta ili kupunguza athari hizo, kuendelea kuyatumia maeneo hayo kwa shughuli za kilimo.
Waziri alisema maeneo ambayo tayari yamejengwa matuta kuzuia maji ya chumvi, ni Koowe, Ukele, Tumbe na Kwa Jibwa iliyopo Kengeja.
Pia, ofisi hiyo imekusanya taarifa za maeneo yote yanayoingia maji ya chumvi Zanzibar, imebaini yapo maeneo 148.
Alisema ofisi hiyo hivi sasa imeanza mchakato wa kutayarisha mapendekezo ya mradi kwa baadhi ya maeneo hayo, ili hatua zinazostahili zichukuliwe.
Fereji alisema kisiwa hicho kinakabiliwa na tatizo la maji ya bahari kuvamia maeneo ya makazi ya wananchi, kutokana na wananchi kukata miti aina ya mikoko kwa matumizi ya ujenzi.
Alisema miti ya mikoko ni maarufu kwa kuzuia kasi ya maji ya bahari kuvamia maeneo ya makazi.
Alisema Serikali imechukua hatua za awali, ikiwamo kutoa ushauri wa kupandwa kwa miti aina ya mikoko pembezoni mwa bahari.
Waziri Fereji alisema SMZ tayari imetafuta mshauri mwelekezi kufanya tathmini ya kina ya athari za mazingira, zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.
Alisema kazi ya mshauri mwelekezi ni kuangalia maeneo ya athari za mazingira, ikiwamo visiwa vidogovidogo ambako wanaishi wananchi.
Waziri huyo alisema Serikali inatarajiwa kupata Sh546 milioni kutoka Mfuko wa Kimataifa wa Mazingira. 
Mwananchi

No comments: