Waziri wa Makazi, Ardhi, Maji na Nishati, Ramadhan Abdallah Shaaban. |
Ramadhan Abdallah Shaaban.Serikali ya Mapinduzi Zanzibar(SMZ), imetangaza mpango wa kuwanyang’anya ardhi vigogo wote waliochukua zaidi ya ekari 10 katika shamba lake la Selem Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Makazi, Ardhi, Maji na Nishati, Ramadhan Abdallah Shaaban, wakati akijibu maswali katika kikao cha Baraza la Wawakilishi kinachoendelea Chukwani mjini Unguja.
Waziri Shaaban alisema serikali imepokea malalamiko kutoka kwa wananchi na baadhi ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, kuwa shamba la serikali ambalo wananchi walikuwa wakilitumia kwa shughuli za kilimo, limechukuliwa na baadhi ya viongozi.Alisema serikali imeshaanza kulifanyia kazi suala hilo na kiongozi yeyote ambaye ametumia zaidi ya eka 10 atalazimika kuacha ekari tano na nyingine kama hizo, kuzigawa kwa wakulima.
Kauli hiyo ya imekuja baada ya Mwakilishi wa Jimbo la Mkwajuni, Mbarouk Wadi Mtando, kuitaka serikali ieleze sababu za kuwanyang’anya wakulima ardhi waliyokuwa wakiitumia kwa kilimo Selem na kuwapa vigogo hao.
Kauli ya mwakilishi huyo iliungwa mkono na Mwakilishi wa Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu, ambaye alisema Mapinduzi ya Zanzibar ya Januari 12, mwaka 1964, yalifanyika kwa lengo la kuondoa matabaka.
Ladhu alihoji sababu za shamba hilo la serikali vigogo wapewe ekari 10 na wananchi wapewe ekari tatu.
Hata hivyo, Waziri Shaaban alijibu kuwa Zanzibar hakuna matabaka bali ni utaratibu wa kawaida ndiyo maana kuna tofauti hata ya mishahara kulingana na heshima ya mtu, hadhi na cheo alichonacho.
Akijibu swali na msingi la Mwakilishi Mwanaidi Hassan Mussa, Naibu Waziri wa Kilimo, Mtumwa Kheir alisema ni kweli baada ya Mapinduzi wananchi waligawiwa ekari tatu tatu za ardhi kwa nia njema ili kuwakomboa wanyonge na kuwaongezea kipato, lakini shamba la serikali la Selem wananchi waliazimwa kwa kazi za kilimo.
Hata hivyo, alisema kwa bahati mbaya baadhi yao walianza kuuza kwa ajili ya makazi kabla ya serikali kuamua kuyagawa mashamba hayo kwa baadhi ya viongozi, jambo ambalo lilipingwa vikali na Mwalikishi Mtando, aliyesema ilipaswa wakulima ndiyo wapewe kipaumbele.
Hata hivyo, alilieleza Baraza la Wawakilishi kuwa mgawo uliofanyika kwa viongozi haukufanyika kutokana na nyadhifa zao, bali walipewa kama wananchi wa kawaida ili wajiendeleze kimaisha kwa kazi za kilimo.
Awali, Mwakilishi Mwanaidi Kassim, alitaka kujua mpango wa serikali wa kuwapatia eneo la ardhi wakulima waliokuwa wakitumia shamba hilo kabla ya kuchukuliwa na kugawiwa kwa vigogo na watendaji wa serikali
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment