ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 10, 2013

‘ Takukuru imetoa funzo’

Kipa wa Simba Juma Kaseja
Dar es Salaam. Wakati Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa Tanzania (Takukuru) ikikosa ushahidi wa kuwafungulia mashitaka ya rushwa wachezaji wanne wa Azam FC, Kipa wa Simba Juma Kaseja amesema hatua hiyo ni fundisho kwa baadhi ya viongozi wa klabu wenye utamaduni wa kuwatupia lawama wachezaji mara timu inapofungwa bila kuwa na ushahidi.
Juzi, Takukuru ilitoa taarifa kushindwa kwake kuthibitisha tuhuma za ulaji wa wachezaji Aggrey Morris, Erasto Nyoni, Said Morad na Deogratis Munishi.
Klabu ya Azam iliwatuhumu na kisha kuwachongea Takukuru wachezaji hao kwa madai ya kupokea rushwa katika mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Simba, ambapo timu hiyo Chamazi ilinyukwa mabao 3-1 kwenye Uwanja wa Taifa Oktoba mwaka jana.
Kaseja amesema kumekuwa na tabia mbaya kwa baadhi ya viongozi na hata watu wa nje kuzusha tuhuma tena bila kuwa na ushahidi dhidi ya wachezaji inapotokea timu imepoteza mchezo.
Awali, Azam iliwashtaki Takukuru wachezaji hao ikiwashutumu kuwa walipokea rushwa ya Sh7 Milioni kwa lengo la kupanga matokeo ya mechi kati ya timu hiyo na Simba iliyopigwa Oktoba mwaka jana.
Akizungumza na Mwananchi jana Dar es Salaam Kaseja alisema: “Ifikie wakati Watanzania tujenge tabia ya kukubali matokeo, haiwezekani timu ikipoteza mchezo tu basi wachezaji watuhumiwe kula rushwa.“Mbona wenzetu hawana tuhuma kama hizi za kizushi?
Timu gani inayoweza kucheza siku zote bila kufunga na ikitokea imefungwa basi wachezaji wamekula rushwa.”
Kaseja aliwataka watu wanaoibuka na tuhuma za rushwa dhidi ya wachezaji wafanye hivyo kabla na siyo baada ya mechi ili wahusika waweze kudhibitiwa mapema badala ya kusubiri hadi pale timu inapopoteza mchezo.
“Kama huna uhakika kwa nini umzushie mwenzako? Kwa nini viongozi wanashindwa kufanya uchunguzi wa kutosha kabla ya kuchukua uamuzi kama uliofanywa dhidi ya wachezaji wa Azam,” alihoji Kaseja.
Wakati Kaseja akisema hayo, Kocha na Mchambuzi wa soka nchini John Kanakamfumu alisema kuwa yeye kilichomshangaza ni kitendo cha Azam kulipeleka suala hilo Takukuru wakati lilikuwa kwenye mamlaka ya klabu hiyo.
“Azam walikosea, kama walikuwa na ushahidi kwa nini walilipeleka Takukuru. Fifa yenyewe imetoa mamlaka kwa klabu kutoa adhabu kwa wachezaji wake, wamekwenda kinyume, wajifunze,” alisema Kanakamfumu.
Wakati huohuo, Katibu mkuu wa Azam, Nassoro Idrissa amewataka wachezaji hao kurejea kwenye kikosi na kuendelea na mazoezi.
Mwananchi

No comments: