Mtoto mmoja ambaye hakufahamika jina lake akiwa amebeba ua katika Mji wa London akielekea katika nyumba ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza Margaret Thatcher, aliyefariki juzi. Picha na AFP
Inadaiwa kwamba alikuwa ni kiongozi katili mpaka akawa anachukiwa na raia wa Uingereza mpaka leo.
London. Mazishi ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa kike wa Uingereza Margaret Thatcher, ambaye aliaga dunia Jumatatu wiki hii, yatafanywa wiki ijayo kwa njia ya kijeshi katika Kanisa la Mtakatifu Paulo.
Kwa sasa bendera za taifa zinapepea nusu mlingoti nchini Uingereza. Wakati huohuo viongozi mbalimbali ulimwenguni wanaendelea kutuma salamu za rambirambi kuhusiana na kifo cha Thatcher.
Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron alituma salamu zake za rambirambi..Naye Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alimtaja Thatcher kuwa ni mmoja wa viongozi wa kipekee ulimwenguni kuwahi kutokea.
Inaelezwa kuwa Thatcher alifariki katika Hoteli ya Ritz iliyoko katikati ya Jiji la London alipokuwa akiugulia.
Thatcher alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 87 kutokana na kuugua ghafla ugonjwa wa kiharusi jana asubuhi nyumbani kwake.
Watoto wa Thatcher, Mark na Carol Thatcher walitangaza kuwa mama yao alifariki kutokana na kuugua kiharusi ghafla adhuhuri ya juzi.
Thatcher aliongoza chama chake cha Conservative katika chaguzi tatu ambazo mara zote chama hicho kiliibuka na ushindi.
Alishika wadhifa wa Uwaziri Mkuu kwa miaka 11 kuanzia Mei 1979 hadi Novemba 1990.
Anakubalika kwa mawazo bora ya kujenga uchumi, ndani na nje ya Uingereza na pia alisifika kwa msimamo wake hasa wa kusonga mbele na kutoyumbishwa na kauli za kukata tamaa.
Kwa sera zake, wapinzani wake waliziita ni za kikatili zilizokuza mwanya kati ya wenye nacho na wasiokuwa nacho.
Ingawa alikuwa mwanamke wa kwanza kuongoza chama kikubwa cha siasa, alipenda kuwakosoa wanaharakati wengi akiwaambia kuwa vita ya haki za mwanamke, ilikwishamalizika na wanawake wameshinda.
Ni mwanamke anayetajwa kuwa na nguvu zaidi kwani ni mwanamke pekee kiongozi wa chama cha siasa ambaye chama chake kilishinda katika chaguzi tatu mfululizo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment