Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), limeshindwa kuzuia utekelezaji wa hukumu ya Mahakama Kuu, iliyoliamuru liilipe fidia Kampuni ya Kufua Umeme wa Dharura, Dowans.
Hatua hiyo, ni baada ya Mahakama ya Rufani kutupilia mbali maombi yake ya kusimamisha utekelezaji hukumu hiyo.
Tanesco iliwasilisha katika Mahakama ya Rufaa maombi ya kusimamisha utekelezaji hukumu ya Mahakama Kuu, ikidai Dola 65 milioni za Marekani, walizoamriwa na ICC kuilipa Dowans ni kiwango kikubwa iwapo kitalipwa itayumba.
Pia, ilidai tayari walishawasilisha nia ya kukata rufaa kupinga hukumu hiyo, huku wakijigamba kuwa wana nafasi kubwa ya kushinda rufaa wanayokusudia kuikata kupinga hukumu ya Mahakama Kuu.
Hata hivyo, uamuzi wa Mahakama ya Rufani uliosomwa jana na Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Elizabeth Mkwizu, ilitupilia mbali maombi ya Tanesco na kuiamuru ilipe gharama za shauri hilo.
Katika uamuzi huo uliotolewa na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya Rufani, walikubaliana na hoja za pingamizi la Wakili wa Dowans, Kennedy Fungamtama, kuwa maombi hayo yaliwasilishwa nje ya muda.
Wakili Fungamtama katika hoja zake za pingamizi alidai kuwa, maombi hayo yamewasilishwa nje ya muda kisheria.
Alidai kuwa kisheria maombi hayo yalipaswa yawasilishwe katika muda wa siku 60 tangu kutolewa kwa hukumu, lakini badala yake Tanesco iliwasilisha maombi hayo baada ya siku 351.
Akizungumzia uamuzi huo, Wakili Fungamtama alisema sasa Mahakama ya Rufani imefungua milango kwa Dowans kukazia hukumu ya Mahakama Kuu ili ilipwe fidia kama ilivyoamuriwa na Mahakama Kuu.
Hii ni mara ya pili kwa Tanesco kushindwa kusimamisha utekelezaji wa hukumu hiyo ya Mahakama Kuu. Kutokana hukumu hiyo itabidi Tanesco kutekeleza amri ya Mahakama Kuu kuilpa Dowans fedha hizo ambazo kutokana na riba zimeongezeka zaidi tangu Mahakama ya ICC itoe hukumu.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment