ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 3, 2013

Vodacom yasaidia mil. 10/- ujenzi kituo cha afya Pemba

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa
 Makame Mbarawa (kulia), akiwaonyesha kazi ya ujenzi 
wa jengo jipya la kituo cha afya kwa Mkuu wa Vodacom 
Foundation, Yessaya Mwakifulefule
Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom kupitia mfuko wake wa kusaidia Jamii (Vodacom Foundation), imetoa Sh. milioni 10 kusaidia kumalizia ujenzi wa kituo cha afya cha Shehia ya Michenzani, Wilaya ya Mkoani Mkoa wa Kusini Pemba.
Jengo hilo linajengwa na Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa akishirikiana na nguvu za wananchi.

Kutolewa kwa fedha hizo ambazo zitanunulia vifaa vya ujenzi vinavyohitajika kwa ajili ya kazi ya kuezeka pamoja na vifaa vingine vya kumalizia ujenzi ni matokeo ya juhudi za mfuko huo za kusaidia miradi ya kijamii yenye lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma za kijamii kwa wananchi hapa nchini.Akikabidhi mfano wa hundi kwa wakazi wa Mkanyageni katika hafla iliyoongozwa na Waziri Profesa Mbarawa, Mkuu wa Mfuko huo, Yessaya Mwakifulefule, alisema Vodacom Foundation imekuwa na dhamira ya dhati ya kusaidia maisha ya Watanzania mijini na vijijini ili kuboresha huduma za kijamii ikiwamo elimu, afya na uwezeshaji wanawake kiuchumi.
Kwa upande wake, Waziri Profesa Mbarawa aliishukuru Vodacom Foundation kwa kukubali kusaidia kumalizia ujenzi wa kituo hicho.
Vodacom Foundation imekuwa ikichangia miradi mbalimbali ya maendeleo Zanzibar ambapo pia hivi karibuni imeahidi kutoa boti mbili za uvuvi kwa vikundi vya vijana Pemba na Unguja kusaidia juhudi za Serikali ya Zanzibar za kutengeza ajira kwa vijana.

Mbali na mchango huo, mwishoni mwa mwaka jana, Vodacom Foundation ilisaidia wanawake wajasiriamali zaidi ya 300 kwa kuwaptia mikopo nafuu isiyo na riba wala dhamana yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 27 katika kisiwa cha Unguja pamoja na kuahidi kuchangia Sh. milioni 15 kwenye mfuko wa maendeleo ya watu wenye ulemavu Zanzibar.
CHANZO: NIPASHE

No comments: