Liwale/Arusha. Uharibifu mkubwa wa mali ulifanywa jana usiku Mjini Liwale, Lindi baada ya wananchi wenye hasira kuchoma moto nyumba za viongozi waandamizi, makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya na maghala ya mazao kutokana na kuchukizwa kushushwa kwa bei ya korosho.
Nyumba zilizochomwa moto ni za Mbunge wa Liwale (CCM), Faith Mtambo, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi cha Umoja, Hassan Myao na Makamu wake, Hassan Mpako, Diwani wa Viti Maalumu (CCM) Liwale, Amina Mnocha, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale, Abbas Chigogola ambaye pia ng’ombe wake tisa walikatwakatwa mapanga na kuachiwa ndama watatu.
Nyingine ni nyumba ya Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Liwale, Mohamed Ng’omambo, Katibu Mwenezi wa CCM Mkoa wa Lindi, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Minali, Mohamed Limbwilindi na Katibu wa chama hicho, Juma Majivuno.
Wakati hayo yakitokea Lindi, huko Arusha, vurugu kubwa za wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu zilizuka jana baada ya kuuawa kwa mwanafunzi Henry Kago (22), juzi usiku.
Wakati hayo yakitokea Lindi, huko Arusha, vurugu kubwa za wanafunzi wa Chuo cha Uhasibu zilizuka jana baada ya kuuawa kwa mwanafunzi Henry Kago (22), juzi usiku.
Kago, ambaye alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa pili, anadaiwa kuwa alifariki jana saa nne usiku baada ya kuchomwa kisu na watu wasiojulikana, akiwa njiani eneo la Kanisa la Wasabato akitokea chuoni hapo kujisomea.
Ghasia za Liwale
Ghasia hizo zilianza jana mchana katika Kijiji cha Liwale B na ziliendelea usiku kucha hadi jana asubuhi.
Ghasia za Liwale
Ghasia hizo zilianza jana mchana katika Kijiji cha Liwale B na ziliendelea usiku kucha hadi jana asubuhi.
Watu walioshuhudia ghasia hizo walisema chanzo ni wakulima kudai kulipwa Sh600 na siyo Sh200 za mauzo ya korosho kwenye Chama cha Msingi Minali.
Bei ya kilo moja ya korosho waliyokubaliana wakulima na chama hicho ni Sh1,200 na mara ya kwanza kiliwalipa Sh600 kwa kilo na kuahidi kulipa nusu nyingine baadaye.
Hata hivyo, viongozi wa Ushirika walibadili uamuzi na kulipa Sh200 kwa maelezo kuwa mauzo hayakuwa mazuri kitendo ambacho kiliwakasirisha wakulima hao ambao waligoma kupokea fedha hizo.
Baadaye ilielezwa kuwa viongozi wa Minali walipeleka fedha hizo polisi ili malipo yafanyike huko, lakini ghasia zikaibuka na wakaamua kusitisha malipo hayo na ndipo wananchi wakaamua kuingia mitaani.
Mmoja wa mashuhuda alisema “Polisi walijaribu kuwadhibiti watu hao, lakini walipoona wanazidiwa nguvu, wakawaachia wafanye wanavyotaka ndiyo maana kumekuwa na uharibifu mkubwa.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, George Mwakajinga alisema kwa kifupi: “Hali imetulia na vurugu zimemalizika lakini bado tuko kwenye kikao kuzungumzia suala hili.”
Wakulima hao walikerwa na tamko la Limbwilindi ambaye ndiye aliyetamka kwamba watalipwa Sh200 kwa kilo na kuamua kwenda kuchoma moto nyumba yake na baadaye ya Katibu wake Majivuno.
Limbwilindi hakupatikana kuzungumzia tukio hilo lakini, Majivuno alipohojiwa alisema: “Tulikubaliana kuwalipa Sh1,200 kwa kila kilo, lakini kwa awamu...
tuliwapa Sh600 awali na nusu yake imeshindikana kwa kuwa mauzo hayakuwa mazuri. Biashara haikwenda vizuri, ndiyo maana tukawaambia tutawalipa Sh200 lakini wakakataa wanataka fedha zote Sh600, sasa sisi hatuna fedha hizo. Kama biashara ingefanyika kwa faida tungewalipa.”
Habari zilizopatikana baadaye leo zilidai kuwa mke wa Mkungura, Amina Mmoto amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Liwale baada ya kupata shinikizo la damu kutokana na sakata hilo.
Akizungumza kwa simu kuelekea Liwale, Mbunge Mtambo alisema: “Nimesikitishwa na ghasia hizi... wamenitia hasara kubwa. Nyumba zangu zote mbili zimechomwa, sijui nitaishi wapi. Hakuna kingine hizi ni siasa tu...hakukuwa na sababu ya kufanya hivyo. Kama ni kulipwa Sh200, mbona vyama vingine wamelipwa fedha hizo na hakukuwa na vurugu?
leo kutwa nzima, Mji wa Liwale ulikuwa na utulivu huku polisi wakitawanya makundi ya watu waliokuwa katika vikundi kwa mabomu ya machozi na shughuli za biashara zilisimama na hakuna maduka wala magenge yaliyofunguliwa.
Vurugu Arusha
Kutokana na vurugu hizo, Chuo cha Uhasibu cha Arusha, kimefungwa kwa muda usiojulikana kwa usalama huku wanafunzi wakitakiwa kuondoka chuoni hapo hadi watakapotangaziwa tena.
Licha ya kuelezwa kwamba aliuawa kwa kisu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo alisema taarifa nyingine, zinaeleza kuwa aliuawa akitokea katika Ukumbi wa Disko wa Bugaloo jirani na chuo hicho.
Baada ya taarifa za kifo hicho, wanafunzi wa chuo hicho walikusanyika leo asubuhi na kuanza maandamano hadi Kituo Kikuu cha Polisi wakilalamikia ulinzi duni.
Mbunge wa Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema alifika na kuwatuliza wanafunzi hao na kuzungumza nao, kwa zaidi ya saa tatu wakati wakimsubiri Mkuu wa Mkoa.
Hata hivyo, baada ya kufika chuoni hapo, mkuu huyo wa mkoa alishindwa kuzungumza kutokana na kutokuwa na kipaza sauti na kusababisha wanachuo kumzomea kabla ya uongozi wa chuo kubadili eneo la mkutano. Hata hivyo, zomeazomea iliendelea na mkutano kuvunjika na FFU kufika na kurusha mabomu ya machozi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo mara baada ya kumalizika kwa Kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama na uongozi wa chuo hicho, mkuu huyo wa mkoa alisema polisi wanafanya uchunguzi wa suala hilo.
“Baada ya kuletewa taarifa za tukio hili na Mbunge Lema, niliondoka na kwenda kuwasikiliza wanachuo lakini tayari nilijua mazingira yalikuwa yamebadilishwa na pale nikagundua Lema ndiyo amekuwa msemaji mkuu badala ya uongozi wa chuo au Serikali ya wanachuo. Ndiyo maana mkaona na zomeazomea ile,” alisema Mulongo.
Alimtuhumu mbunge huyo uchochezi na ameamuru kukamatwa kwake na wanafunzi waliohusika na vurugu zile.
Lema alieleza kusikitishwa na agizo la kutakiwa kukamatwa akisema alizuia maandamano kufika mjini... “Nyie waandishi wa habari mlikuwepo nimezungumza zaidi ya saa mbili na wale wanafunzi kuwasihi watulie wasiandamane na mimi ndiye nilimpigia simu Mkuu wa Mkoa aje kuwasikiliza wanafunzi iweje niwachochee kufanya fujo? Ninawasubiri waje wanikamate.”
Mwananchi
No comments:
Post a Comment