ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 23, 2013

DPP sasa akata rufani Lwakatare kufutiwa ugaidi

Dar es Salaam. Kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare na mwenzake, Joseph Ludovick Rwezaura, sasa imetua Mahakama ya Rufani, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuiomba mahakama hiyo kuingilia kati.

Lwakatare na Rwezaura, walikuwa wakikabiliwa na kesi ya ugaidi katika Mahaka
ma ya Hakimu Mkazi Kisutu, lakini Mahakama Kuu iliwafutia mashtaka hayo na kubaki na shtaka la kula njama.
Hata hivyo, DPP amewasilisha maombi ya marejeo Mahakama ya Rufani akiomba iitishe majalada ya kesi hiyo na kuchunguza uhalali wa uamuzi wa Mahakama Kuu wa kuwafutia mashtaka ya ugaidi.Katika maombi yaliyowasilishwa na DPP, anaiomba Mahakama ya Rufani ifute uamuzi na amri za Mahakama Kuu, kuhusu uhalali wa mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili washtakiwa.
DPP, katika maombi hayo anadai washtakiwa walikuwa hawajaitwa kujibu mashtaka na kwamba, kwa hali hiyo haikuwa sahihi Mahakama Kuu kuamua kuwa mashtaka hayo hayakuwa halali. Pia, anadai kuwa katika maombi ya washtakiwa Mahakama Kuu, hapakuwapo na maombi ya kufuta mashtaka. DPP anaongeza katika maombi hayo kuwa, hapakuwa na taarifa zilizowasilishwa dhidi ya washtakiwa, ambazo Mahakama Kuu ingezizingatia kuamua uhalali wake, au kuwapo kwa upungufu.

Hivyo anaomba Mahakama ya Rufani ione kuwa uamuzi wa Mahakama Kuu kufuta baadhi ya mashtaka kwenye hati ya mashtaka ya awali, yaliyokuwa yakiwakabili washtakiwa hao haukuwa sahihi.
Lwakatare na Rwezaura walikuwa wakikabiliwa na mashtaka manne, matatu kati ya hayo yakiwa ya ugaidi na moja la kawaida la jinai, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Walikuwa wakidaiwa kula njama na kupanga kumteka Dennis Msacky, kisha kumdhuru kwa kutumia sumu.
Hata hivyo, Mei 8, mwaka huu Jaji Lawrence Kaduri wa Mahakama Kuu aliwafutia mashtaka ya ugaidi na kuwabakizia linalohusu jinai ya kula njama za kutenda kosa la kumdhuru Msacky kwa kutumia sumu.

MWANANCHI

No comments: