ANGALIA LIVE NEWS

Friday, May 24, 2013

KAMA UNATAKA FURAHA, FUATA MTINDO HUU WA MAISHA!

KUWA na msongo wa mawazo, hasira, chuki na mengine yanayofanana na hayo ni hatari kiafya. Wakati mwingine unaweza kushindwa kufanya mambo mengine kwa sababu ya kutumia muda mwingi kufikiri juu ya mambo hayo.

Yote hayo yanaweza kuingia katika moyo wa mwanadamu ikiwa mtindo wake wa maisha hautakuwa mzuri. Kwa sababu hapa nazungumzia kuhusu mapenzi nitakwenda moja kwa moja kwenye eneo hilo.
Matatizo hayo mara nyingi husababishwa na kero katika uhusiano. Ni vizuri kuangalia namna bora ya kuishi na mpenzi wako ili uweze kutengeneza furaha ya kudumu katika maisha yako.
Lakini jambo kubwa la msingi la kujiuliza hapa, ni kwa nini watu wanaingia kwenye migogoro ya mapenzi? Jibu lake ni jepesi sana. Ni kwa sababu mtindo wa maisha yao ni mbaya.

ISHI KIRAFIKI
Ukitaka kuufanya uhusiano wako usilegelege jifunze kuishi kirafiki na mwenzi wako. Hapa wanaume wengi ndiyo tatizo. Baadhi yao huwa wanapenda kuwa wababe wakati wote bila sababu ya msingi.
Kuishi na mwenzako kibabe haifurahishi na uhusiano lazima utakuwa na migogoro. Usimfanye mwenzako akuogope, ahisi wewe ni mkali muda wote, pengine hadi pale mtakapokutana kwa ajili ya tendo tu ndipo furaha ya muda hupatikana.
Pendelea kuwa karibu na mpenzi/mke wako. Wapo rafiki zangu wengine hawawezi hata kutembea na wanawake (hasa walio kwenye ndoa) zao barabarani. Wapo ambao wanafikia hatua ya kumtanguliza mwenzake, halafu yeye anafuatia nyuma!
Shida yote ya nini? Kwa nini ulimchagua kama hujiamini ukiwa naye? Kuwa karibu na mwenzako, tembea naye barabarani tena kwa upendo huku mkiwa mmeshikana mikono.
Kufanya hivyo kutamfanya ajiamini yupo na mwanaume anayempenda. Kwa kiasi kikubwa, jambo hili litasaidia sana kuziba mwanya wa mwenzako kuanzisha ugomvi ambao hauna maana. Ugomvi utatokea wapi mahali penye maelewano na amani?
Kwa wanandoa ni vizuri kulala katika mtindo wa kukumbatiana au kusogeleana kwa karibu. Hii itawafanya wote kwa pamoja kuhisi joto la mwingine.
Huu ni uchawi mkubwa sana katika mapenzi. Kuwa karibu kunawafanya wote mjione kuwa ni sehemu ya maisha ya mwingine hivyo kuziba mwanya wa kutofautiana.

SAMEHE NA KUSAHAU
Hakuna mtu aliyekamilika, kila siku tunakosea hivyo ni vyema kujenga mazoea ya kumsamehe mwenzako kwa moyo wote. Si kusamehe tu bali unapomsamehe mwenzio pia usahau tatizo hilo.
Kusamehe na kusahau ni chachu ya mapenzi, huwezi kuwa na kinyongo na muda wote utakuwa mwenye furaha. Wiki ijayo tutaendelea, USIKOSE!

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Mambo ya Mapenzi anayendikia Magazeti ya Global Publishers. Ameandika Vitabu vya True Love, Let’s Talk About Love na All About Love vilivyopo mitaani.

No comments: