Mkurugenzi Mkuu wa SSRA, Irene Isaka, aliitaja mifuko hiyo kuwa ni wa Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma (PPF) na ule wa Hifadhi ya Jamii (NSSF).
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, kuhusu Maonyesho ya Wiki ya Hifadhi ya Jamii yatakayofanyika mkoani Dodoma kuanzia Mei 13 hadi 18, mwaka huu katika viwanja vya Nyerere Square, Isaka alisema wanachama wengi wamekuwa wakienda kuchukua mafao yao kabla ya kufikisha umri wa kustaafu, hasa baada ya sheria kuwaruhusu kufanya hivyo.
“Wanachama wanajitoa sana hasa kwenye mifuko ya PPF na NSSF, wanaenda kuchukua mafao. Tunafanya uchunguzi kujua kwa nini hili linatokea kwa sababu kuna taarifa kwamba baadhi ya waajiri wanashirikiana na wafanyakazi kuwaandikia barua za kuacha kazi ili wapate mafao yao,” alisema.
Hata hivyo, bila kueleza ni wanachama wangapi wamejitoa kwenye mifuko hiyo, Isaka alisema kasi hiyo ina manufaa ya muda mfupi kwa mwanachama kuliko faida ya kupata mafao mazuri baada ya kustaafu.
“Kasi ya kujitoa ni mbaya na yanayotokea PPF na NSSF ni kutumia vibaya fursa ya kuchukua mafao iliyotolewa,” alisema Isaka.
Alisema katika kujitoa huko, Mkurugenzi mmoja ambaye hakumtaja jina alishangaa kupelekewa hundi ya malipo ya mfanyakazi wake ambaye bado yuko kazini, jambo lililomshtua na kuamua kupiga simu kwenye mfuko husika kuhoji sababu za kumlipa mfanyakazi wake mafao ilihali bado yupo kazini.
Alisema tukio hilo lilimaanisha kwamba baadhi ya mameneja rasilimali watu ndiyo wanaoandika barua za kuthibitisha mfanyakazi ameachishwa kazi wakati siyo kweli.
“Ndiyo maana tunasema tutafanya uchunguzi kujua kwa nini hali hii inatokea, napenda tu niwakumbushe wafanyakazi, ukishachukua fao kwenye mfuko mmoja huwezi kuhama, hata ukiachishwa kazi, ukipata nyingine utalazimika kukaa kwenye mfuko huo huo,” alisema.
Hata hivyo, aliwatoa hofu wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii na kueleza kwamba iko salama na ina uwezo wa kuendelea kutoa mafao bila matatizo.
Isaka alisema hivi sasa SSRA inatengeneza miongozo mbalimbali ya kuwianisha mafao ili wanachama waweze kupata mafao mazuri kuliko ilivyo sasa kwani baadhi ya mifuko inatoa mafao mazuri maradufu ya mingine.
Alisema mwongozo mwingine ni ule wa uwekezaji ili mifuko iendelee kufanya uwekezaji wenye manufaa.
Kwa mujibu wa Isaka, mwongozo mwingine ni ule wa uundaji wa bodi za wadhamini na sifa za wajumbe wa kuziunda.
Aliitaka pia mifuko iwe inatoa taarifa sahihi kwa wanachama wake na kwamba wasitoe takwimu za uongo kinyume cha hali halisi ya mfuko kwa nia ya kuwafurahisha wanachama.
Alisema mifuko yote imeanzisha mifuko ya hiari ambayo inatoa fursa kwa wananchi wote kupeleka michango yao kwenye mifuko hiyo hata walio katika sekta isiyo rasmi.
Akizungumza na NIPASHE, Kaimu Meneja Kiongozi wa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa NSSF, Theopista Muheta, alithibitisha kwamba kumekuwa na kasi kubwa ya wanachama kujitoa kwenye mfuko huo.
Alisema baadhi ya wanachama wanahofia kwamba serikali inaweza kutunga sheria ya kuzuia fao la kujitoa.
Hata hivyo, alisema hakuwa na takwimu za hali halisi kuhusu kasi hiyo.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano wa PPF, Lulu Mengele, alisema asingeweza kuzungumzia hali hiyo kwa kuwa tayari SSRA imekwishazungumza vizuri.
Kujitoa huko kumekuja miezi michache baada ya serikali kuridhia kuondoa zuio la fao la kujitoa baada ya wafanyakazi na baadhi ya wabunge kulalamikia sheria ya Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2012, inayozuia wanachama kujitoa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii hadi wafike umri wa miaka 55 na 60.
Baada ya mvutano wa muda kati ya wabunge na serikali ambayo iliwasilisha bungeni muswada wa sheria hiyo uliokuwa unazuia fao la kujitoa, muswada huo ulirekebishwa na sasa mifuko yote itaendelea kutoa fao hilo kama ilivyokuwa kabla ya zuio hilo na kwa vigezo vile vile kwa wanachama wanaostahili kupata fao hilo.
Wakati huo huo, maonyesho ya wiki ya hifadhi ya jamii ambayo yatafanyika mkoani Dodoma yatafunguliwa na Rais Jakaya Kikwete na yatafungwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudentia Kabaka.
Isaka alisema maonyesho hayo yatakwenda sambamba na upimaji wa afya bure kwa wananchi watakaotembelea maonyesho hayo.
Alisema pia mifuko itatoa misaada ya kijamii katika nyumba ya watoto wenye mtindio wa ubongo ya Miyuji na katika Hospitali ya Mkoa wadi ya Chikande.
CHANZO: NIPASHE
1 comment:
mie ni mlinzi utanambia vp nilinde hadi miaka 55???????????? huo ni uonefu sana chamsingi we mkurungenz una hekima, umesoma, sidhani kama sisi utakua unatutendea haki hata kidogo. kama una muogopa Mungu nakumba aacha hilo swala make anaeumia ni mtu wa chini sana. huo sio uungana hata tumia elimu yako vizuri
Post a Comment