Advertisements

Tuesday, May 7, 2013

UTAMU AU MATESO YA MAPENZI HUTOKANA NA MTINDO WAKO WA MAISHA - 5

MAPENZI siku zote yanakutaka upate furaha badala ya mateso, ndiyo maana kuhakikisha hilo linatimia, wiki iliyopita nilikutaka ujiangalie wewe mwenyewe. Unapojisikia huna furaha, mara nyingi inakuwa rahisi kuwaza kuna tatizo kwenye uhusiano wako kitu ambacho siyo sahihi.

Utamlaumu mwenzako kuwa yeye ni sababu ya wewe kutokuwa na furaha. Bahati mbaya zaidi ni kwamba unaweza kudhani kuwa suluhisho lipo ndani yake. Hilo ni kosa kubwa, hata kama ni kweli yeye ndiye anakunyima raha, hebu mwoneshe kuwa unaweza kuyafurahia maisha bila yeye.

Kwanza, unapowaza kuwa mwenzi wako ndiye suluhisho, unamfanya ajione ana mamlaka makubwa sana juu yako. Pili, hutapata ufumbuzi wa majanga yanayokusibu kwa sababu unakuwa hujapata mzizi wa tatizo. Penda kuusaka mzizi wa tatizo na hilo ni jukumu lako mwenyewe!

Siku yoyote ile, ikiwa unajisikia kumlaumu mwenzi wako kutokana na hisia ulizonazo, kwamba iwe kuna kitu amefanya au hajafanya kile ambacho unadhani alipaswa kufanya, jaribu kwanza kujiuliza na kujitazama wewe kwa makini kabisa. Tatizo limetokea, hebu liangalie kwa upande wako.

Kujiuliza ukiwa umetulia, kuna sauti ya ukweli sana huwa inanong’oneza. Hiyo itakwambia hali halisi ya tatizo. Bahati mbaya nyingine ni kwamba wengi huwa wanaikataa kwa sababu huwashambulia wao wenyewe. Lazima tukubali kukosolewa kama kweli tunataka furaha ya maisha yetu.

Huna raha lakini kila siku unaelekeza lawama kwa mwenzi wako, wakati makosa yapo kwako wewe mwenyewe. Sauti ya ukweli ndani yako inakwambia, unaipinga na kushikilia misimamo ambayo siku zote inapoteza. Ubishi hautakusaidia katika maisha yako, sanasana utakuharibia furaha yako.

Katika uhusiano, kuna pande mbili. Wewe unaweza kuamua kushikilia furaha yako ambayo itakufanya uwe na amani, ukilalia upande wa pili, huko kuna mateso, majuto na majanga yasiyokwisha. Chukua hatua kamilifu leo, ukubali ukweli pale makosa yanapoonekana upande wako ili maisha yasogee.

Katika hili, kuna hekima moja kubwa sana. Ni kwamba hata kama tatizo lipo kwa mwenzi wako, suluhisho linaweza kupatikana kwa wewe mwenyewe bila kumshirikisha. Angalia ni kipi ulifanya, ukamsababishia naye kutenda hicho kinachokunyima raha. Ukishakitambua, chukua hatua haraka.

JITAMBUE NA USIJIKATAE
Ni kosa kubwa kupingana na ukweli. Vivyo hivyo, utajikuta unakosa furaha na hauna amani kabisa kwa sababu ya kutojitambua. Kama una tabia ya kupuuza simu na SMS za mwenzi wako, usikimbie tatizo, unatakiwa ujikubali kwamba hiyo ni kasoro iliyo ndani yako ili muweze kwenda vizuri.

Kuna watu wana kawaida ya kuzikataa sifa walizonazo na kutaka kuwabebesha wengine. Mathalan, wewe ni mbishi sana na ubishi wako umekuwa ukisababisha malumbano yasiyokwisha kwa mwenzi wako. Hutapata ufumbuzi kama hutajitambua, ukijikataa ni mzigo wako mwenyewe na utakutesa kila siku.
Wakati mwingine ni kazi ngumu kujitambua lakini itakupa unafuu mkubwa kama utakapofanikiwa huo mtihani. Utaepukana na mzigo wa kuwalaumu wengine, utajikuta upo huru kuliko ambavyo unaweza kuwaza na kupata jibu hivi sasa. Lifanyie kazi suala hili kwa mafanikio yako ya baadaye.

Wala haitakuumiza na ukidhamiria ni kitu rahisi. Wakati ujao, likitokea tatizo la aina yoyote, kabla hujamshushia lawama mwenzako, angalia ukweli uliopo ndani yako. Je, hakuna kosa la upande wako? Jibu utakalopata ndilo ambalo litakuwezesha kuingia kwenye dunia ya furaha na mapenzi yenye utamu na siyo mateso.

Itaendelea wiki ijayo.

Global Publishers

No comments: