ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, May 12, 2013

KWA NINI UWE NA ROHO YA KWA NINI MWENZAKO ANAPOFANIKIWA?

KAMA wewe ni mfuatiliaji wa safu hii utakubaliana nami kuwa mara kadhaa nimekuwa nikizungumzia mafanikio. Msisitizo wangu katika hilo ni kwamba kila mmoja wetu anayo nafasi ya kufanikiwa endapo ataamua na hata kwenye makala ya wiki iliyopita utakumbuka sikuwa mbali sana na hiki nitakachokizungumza leo.

Hakuna watu waliochaguliwa na Mungu kwamba wao ndiyo watakaofanikiwa tu na kwamba wengine wataishi katika ufukara kwa maisha yao yote. Hakuna kitu kama hicho!
Kimsingi kila aliyefanikiwa aliamua kufanikiwa na kwa maana hiyo kila anayetaka mafanikio na kapambana vilivyo, hakuna kipingamizi, mafanikio ni lazima yatapiga hodi kwenye maisha yake.

Wakati uhalisia ukiwa hivyo, kuna watu huko mtaani naweza kusema ni wa ajabu sana. Hawa ni wale wenye roho ya kwa nini wanapowaona watu walio karibu yao wakipata mafanikio katika maisha yao.
Eti wanaumia sana na wakati mwingine wanadiriki kujenga chuki dhidi yao kwa kigezo kwamba wanaringa ama wanajisikia kwa mafanikio waliyoyapata. Wao hawataki kabisa kuwaona wenzao ama watu wanaowafahamu wakipata mafanikio.

Utafiti unaonesha wengi wamekuwa wakichukizwa sana wanapowaona wale ambao wako nao karibu wakipiga hatua katika maisha lakini ikitokea mtu ambaye hawamjui kabisa wala hawana uhusiano wowote akafanikiwa huwa hawaumii.

Huwa najiuliza sana juu ya hili. Labda nikuulize wewe msomaji kwamba unadhani ni kwa nini sisi binadamu tunakuwa na roho za kwa nini, chuki na kijicho kwa wengine hasa wanapofanikiwa badala ya kuwapongeza na kuchukulia kwamba kufanikiwa kwao ni changamoto kwetu? 

Ninachoona hapa ni kwamba kuna hali fulani ya ubinafsi, hali ya umimi ambayo inatujengea mazingira ya kujipenda sisi wenyewe kuliko wengine. 

Tunaona sisi tu ndiyo tunastahili kufanikiwa na siyo wengine ndiyo maana inapotokea kinyume chake tunaumia sana.

Zaidi ya hivyo inaonekana kwamba wengi wetu tunatamani sana kusifiwa na kuonekana kwamba ndiyo wenye thamani na bora kuliko wengine.Huu ni ulimbukeni uliopitiliza.
Itaendelea wiki ijayo.
GLP

No comments: