Mwanaume anatakiwa kuwa makini na mwenzi wake wakati wa hisia za kipindi cha mpito, vilevile mwanamke naye anapaswa kujichunga. Hisia zake, hazitakiwi kumpeleka mahali ambapo anaweza kumsaliti mwenzi wake au ndoa yake.
Wengi walijuta sana baadaye, baada ya kugundua kwamba wanaume ambao waliwavuta na kuwaona ni bora sana kwa sababu waliwafariji, ni majanga mtindo mmoja. Ukweli ni kuwa mwanzoni anapokuja kwako, hawezi kukuonesha tabia zake za ajabu, daima atakufanya umuone ni mtu bora sana.
Hivyo basi, usingoje kujuta baadaye, kwani majuto ni mjukuu. Amua kumkataa mwanaume anayekuja kukufariji leo kwa sababu una matatizo, badala yake mkumbushe mwenzi wako awe jirani na wewe, kwani unahitaji faraja yake kwenye kipindi hiki kigumu ulichonacho.
Kwa mwanaume, pigana kila siku kuhakikisha mwenzi wako hatekwi na hisia za mpito. Unampenda, kwa hiyo ni wajibu wako kumlinda. Kumweka mbali na majaribu. Anaweza kukusaliti na baadaye ukamwita malaya, wakati makosa yapo pia upande wako kwa sababu ulimweka mbali alipokuwa anahitaji uwepo wako.
Mwanamke anapozidi kukua, umri kuongezeka, anapopoteza wazazi au wigo wake wa kiuhusiano kwenye jamii unapopanuka, moja kwa moja hujikuta yupo kwenye majaribu. Unapaswa kuwa wa kwanza kumsoma, kujua nyakati aliyopo na kuchukua uamuzi wa kumuokoa.
Nilishaeleza kuhusu mahitaji ya ndoa na namna ambavyo yanavyoweza kumlazimisha mwanamke kumsaliti mwenzi wake. Kimsingi, mwanamke anapokuwa ameweka matarajio yake mbele na akiwa anahitaji kuyatimiza, ni rahisi kusaliti. Chunga akilini mwako.
Anahitaji kufaulu, anaweza kufanya lolote kuhakikisha ndoto zake zinatimia. Ni mke/mchumba/mpenzi wa mtu lakini anaweza kujikuta anatoa penzi kwa mwanafunzi mwenzake au mhadhiri wa chuo kwa sababu tu anataka kufikia malengo yake.
Jitahidi sana kumuweka karibu mwenzi wako kujua mahitaji ya wakati. Ukishatambua kile anachokitaka, hakikisha unamtimizia kama kipo ndani ya uwezo wako, ikiwa kipo juu yako, basi fanya hima kuwa jirani naye, kufanya hivyo, utakuwa umemuepusha na vishawishi visivyo na lazima.
HISIA HASI KIPINDI CHA SHEREHE
Mwanamke huhitaji pongezi anapofanya jambo zuri. Siku zote hutaka mwenzi wake ndiye awe wa kwanza kumpongeza kwa mafanikio yoyote anayoyapata. Inapotokea hapati kile anachokitarajia kutoka kwa mume/mchumba/mpenzi wake ni hapo maumivu mengi ya ndani kwa ndani humzingira.
Kila anayeumia, huhitaji faraja ili ajipoze. Sasa basi, wewe unapokaa mbali naye, ukaweka kinyongo kwa mafanikio yake, mwisho humsababisha amuone mwingine ambaye anaweza kusherehekea naye. Hicho ni kipindi ambacho, nafasi yako ya kusalitiwa ni kubwa mno.
Amefaulu mtihani, amepata kazi au amepandishwa cheo kazini kwake, wewe ndiye unaweza kukamilisha sherehe yake. Unapaswa kuhakikisha anakuona wewe ni sehemu ya mafanikio yake. Kitendo cha kumpongeza kwa maneno, kumkumbatia au kugonga glasi na kusherehekea pamoja, hufanya ajione mwenye furaha iliyotimia.
Itaendelea wiki ijayo.
GPL
No comments:
Post a Comment